Mwanafunzi wa kiume anayesoma darasa la sita (shule haijatajwa) kutoka Kaunti ya Garissa nchini Kenya amezua kasheshe baada ya kumshambulia mwalimu wake kwa kisu mara baada ya kuulizwa kwanini amekua mtoro.
Kwa mujibu wa televisheni ya Citizen ya Kenya inadaiwa baada ya mwalimu wake kumuuliza hivyo huku akiongea kwa msisitizo ulizuka mzozano, baadaye mwanafunzi aliondoka darasani na kurejea akiwa na kisu ambacho alikitumia kumchoma mwalimu huyo sikioni.
Baada ya tukio hilo inataarifiwa kwamba mwalimu huyo mwanamke alijeruhiwa vibaya na kukaribia kupoteza uwezo wake wa kusikia.
Akizungumza na wazazi Kamishina wa Polisi wa kaunti hiyo, Boaz Cherutich amewaonya wanafunzi kutowashambulia walimu shuleni akisema watakaopatikana na hatia watakabiliwa na mkono wa sheria.
Aidha amewataka wazazi na walimu kushirikiana ili kupunguza matukio ya utovu wa nidhamu shuleni.
Cherutich pia alisema kuna wakuu wa shule kadhaa katika eneo hilo wameomba kuhamishwa kufuatia vitisho kutoka kwa wanafunzi wao kila wanapojaribu kuwarekebisha.
Chanzo: Mwananchi