Na Mwandishi Wetu,
MENEJA Miliki wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Alexander Ndibalema amesema miundombinu yote muhimu na wezeshi kwa ajili ya kuhudumia makasha (makontena) katika bandari kavu ya Kwala iliyopo iliyopo wilayani Kibaha mkoani Pwani imeshakamilika.
Hivyo bandari hiyo kavu kuwa na sifa zote na tayari kwa kuanza kazi huku akisisitiza tayari bandari hiyo imeshasimikwa mifumo ya kimatandao ambayo inasomana moja kwa moja na bandari ya Dar es Salaam
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari leo Ndibalema amesema pia tayari katika bandari hiyo zipo ofisi za wadau wote bandari pamoja ofisi za kiforodha.
Bandari ya Kwala itakuwa ni mahususi kwa ajili ya kuhudumia makasha (makontena) yanayokwenda nchi jirani na imeunganisha nchi jirani lengo likiwa ni kuhudumiwa makasha (makontena) yanayokwenda nchi jirani.
"Tayari tumeshatenga maeneo maalum kwa kwa ajili ya nchi za Burundi, Rwanda, DR Congo ambapo kila nchi zimetengewa hekta kumi (10), " amesema na kuongeza malengo ya kujenga bandari hiyo kuwa ni pamoja kupunguza msongamano wa mizigo na malori katika Bandari ya Dar es Salaam.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha Kwala, Zaka Msafiri amesema, ujio wa bandari kavu ya Kwala imewanufaisha wakazi wa Kwala na maeneo jirani katika nyanja mbalimbali.
Mwenyekiti Msafiri ameyataja baadhi ya manufaa hayo kuwa ni pamoja na wananchi kupata ajira, kukuza biashara ,kuvutia uwekezaji pamoja na kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kufuatia barabara yenye urefu wa kilometa 15.5 kujengwa ikiwa pia ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa bandari hiyo.
Kwa upande wao wa wananchi wa Kijiji cha Kwala Robert Francis na Jumanne Kibambe wameishukuru serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza kwa kasi miradi yote muhimu na ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa bandari kavu ya Kwala.
Meneja Miliki wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) , Alexander Ndibalema akiwaelezea waandishi wa habari juu ya ulipofikia mradi wa ujenzi wa bandari kavu ya Kwala iliyopo iliyopo wilayani Kibaha mkoani Pwani leo Mei 27, 2023
Mwonekano wa vifaa kazi mbalimbali vilivyopo katika bandari ya Kwala kama vilivyokutwa na mpiga picha wetu leo Mei 27, 2023
Mwonekano wa ofisi za wadau wa bandari ambazo zimekamilika katika bandari kavu ya Kwala kama zilivyokutwa na mpiga picha wetu leo Mei 27, 2023
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Kwala akiongea na waandishi wa habari leo Mei 27, 2023