Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Jangwa la Sahara,Tawi la Tanzania (MISA Tanzania), inaadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake,MISA ilizaliwa mwaka 1992 baada ya kikao cha wanahabari waliokutana Windhoek,Namibia kujadili mambo mbalimbali yaliyokuwa yanaukabili Ukanda wa Nchi za Kusini.
MISA ina matawi tisa katika nchi za Zambia, Msumbiji, Malawi, Eswatin, Botswana, Namibia, Angola, Tanzania na Zimbabwe ambako ndiyo makao makuu ya matawi yote.
Kwa mwaka huu,MISA Tanzania inaazimisha miaka 30,kwa kuangalia ilitoka,iliko na inakokwenda hasa kwa kuangalia namna inavyotekeleza majukumu yake ya msingi ambayo ni Uhuru wa Kujieleza, Upatikanaji wa Taarifa na uhuru wa vyombo vya habari.
Maadhimisho haya yanafanyika Jijini Dodoma na kuwaleta pamoja wanachama,viongozi na watendaji wa MISA-TANZANIA pamoja na wadau wa Habari na washirika wake wa ndani na nje ya nchi (zaidi ya 100 kwa idadi); wakiwamo MISA makao makuu.
Kwa ajili ya kufanya tafakuri na kuwa na mwelekeo mzuri katika kuleta mabadiliko katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya kuhabarisha umma.
Katika mkutano huo wa siku mbili wadau watajadiliana kuhusu kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia na namna ambavyo umma unahusishwa kwenye uhuru wa kujieleza na upatikanaji wa taarifa.
Pia wataajadili changamoto zilizopo kwenye sekta ya habari na kuweka mkakati wa kuzitatua ikiwamo namna ya kuboresha maisha ya waandishi wa habari.
Pamoja na hayo, majadiliano haya yana malengo ya kuongeza ukaribu kati ya waandishi wa Habari na jamii, kuibua miradi itakayo wakutanisha zaidi jamii na waandishi wa Habari, kuibua mpango kazi wa utekelezaji ili kuhakikisha kila mwanajamii anatumia vizuri nafasi ya uhuru wa kujieleza kuita vyombo vya Habari kwaajili ya maendeleo endelevu.
Tunatarajia mgenj rasmi atakuwa Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mh. Mha. Kundo Mathew. Kauli mbiu ya mwaka huu ni "Uhuru wa Kujieleza Msingi wa Haki Zote kwa Maendeleo Endelevu"