Breaking

Saturday, 27 May 2023

MFUMO WA UFUATILIAJI HALI YA BARABARA WAFIKIA WANANCHI ELFU 15

Imeelezwa kuwa zaidi ya wananchi 15,000 tayari wameingia kwenye mfumo wa kielektroniki wa ufuatiliaji wa hali ya barabara na kutoa taarifa au changamoto mbalimbali wanazo kutana nazo wanapotumia barabara katika maeneo mbalimbali nchini.

Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki na Kaimu Meneja Mfuko wa Barabara Eng. Rashid Kalimbaga wakati akiongea na waandishi wa habari katika viwanja vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma, ambako Bodi ya Mfuko wa Barabara imeweka kambi kwa ajili ya kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mfumo huo kwa wabunge.

“Kwa upande wa taarifa tulizopokea tangu mfumo huu umezinduliwa mwezi Julai mwaka 2022 jijini Mwanza tayari tumepokea taarifa zaidi ya 15,000. Taarifa 9,300 ambazo ni sawa na asilimia 62 ya taarifa zilizotolewa tayari zimefanyiwa kazi na ambazo bado zinafanyiwa kazi ni taarifa 5,700 sawa na asilimia 18. Kwa hivyo utaona kwamba ni mfumo ambao unafanyakazi, taarifa zinakuja na zinafanyiwa kazi na mwananchi ambae anatoa taarifa anapatiwa mrejesho kwa wakati. kulingana na tatizo aliloliripoti”. Amesema Mhandisi Kalimbaga.

“Taarifa hizi zinahusu hasa hali ya barabara kwa mfano kumetokea dharura kalavati limezolewa na mafuriko ya mvua, barabara imekatika, uwepo wa shimo barabarani au thamani za barabara zimeibiwa basi wananchi wanaweza kutoa taarifa ya hali hiyo kupitia simu za mkononi, na taarifa hiyo itafika moja kwa moja kwa wakala wa barabara husika na watachukua hatua na kuitolea mrejesho kwa mtoa taarifa”. Ameongeza Mhandisi Kalimbaga.

Mhandisi Kalimbaga amesema kuwa Bodi ya Mfuko wa Barabara imeamua kuweka kambi ya Bungeni hapo ili kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mfumo huo wa kielektroniki wa ufuatiliaji wa hali ya barabara kwa wabunge ili nao wakishauelewa wasaidie kutoa elimu kwa wananchi majimboni mwao hali itakayosaidia kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa haraka na hivyo kuongeza ulinzi kwenye miundombinu ya mtandao wa barabara nchini.

Kwa upande wake Mhandisi Jacob Mukasa kutoka Bodi ya Mfuko wa Barabara amesema kuwa mfumo huo ni rahisi kutumika na kila mwananchi kwa kuwa unapatikana kupitia simu za mkononi kwa kupakua mfumo huo uitwao Barabara kupitia App Store au Play Store, au kwa kubonyeza *152*00# na kuchagua namba nne halafu tano na kisha kufuata maelekezo ya kutoa taarifa za hali ya barabara.

Bodi ya Mfuko wa Barabara iliunda mfumo huo kwa kutumia wataalamu wake wa ndani ili kuwashirikisha wananchi katika ufuatiliaji wa hali ya barabara na hivyo kuongeza ulinzi wa miundombinu ya barabara ambayo Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuijenga. Tunza Barabara, Zikutunze.

Imetolewa na Bodi ya Mfuko wa Barabara
Mbunge wa Jimbo la Ushetu Emmanuel Cherehani (kulia), akiteta jambo na Kaimu Meneja Mfuko wa Barabara Mhandisi Rashid Kalimbaga (Kushoto) pamoja na Mhandisi Jacob Mukasa wa Bodi ya Mfuko wa Barabara, baada ya kufurahishwa na huduma ya utoaji elimu ya matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa ufuatiliaji wa hali ya barabara Bungeni jijini Dodoma.




Watoa elimu ya matumizi sahihi ya mfumo wa kieletroniki wa ufuatiliaji wa hali ya barabara Comfort Mgarula (kushoto) na Bi Segolena Francis (wa pili kulia) kutoka Bodi ya Mfuko wa Barabara, wakitoa elimu hiyo kwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ghati Chomete (kulia) na Santiel Kirumba (wa pili kushoto), Bungeni jijini Dodoma
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Moshi Kakoso (Kushoto), akipata elimu ya matumizi sahihi ya mfumo wa kieletroniki wa ufuatiliaji wa hali ya kutoka kwa Eng. Jacob Mukasa wa Bodi ya Mfuko wa Barabara, Bungeni jijini Dodoma mwishoni mwa wiki
Mbunge wa Bunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Fransis Ndulame (Kushoto), akisalimiana na Kaimu Meneja Mfuko wa Barabara Eng. Rashid Kalimbaga wakati wa zoezi la utoaji elimu ya matumizi sahihi ya mfumo wa kieletroniki wa ufuatiliaji wa hali ya barabara inayotolewa na Bodi ya Mfuko wa Barabara, Bungeni jijini Dodoma.

Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Eng. Leonard Chamuriho (kushoto) na Eng. Mwanaisha Ulenge (kulia), wakitoa maoni yao baada ya kupata elimu ya matumizi ya mfumo wa kieletroniki wa ufuatiliaji wa hali ya barabara inayotolewa na Bodi ya Mfuko wa Barabara, Bungeni jijini Dodoma. Wengine ni Eng. Jacob Mukasa (kushoto kwa Chamuriho) na Msitiri Malongwe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara.


Picha na Bodi ya Mfuko wa Barabara

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages