Breaking

Thursday, 4 May 2023

MANISPAA YA SHINYANGA YAIMARIKA UKUSANYAJI MAPATO, YAPONGEZWA KASI UTEKELEZAJI MIRADI


Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Mhe. Elias Ramadhani Masumbuko akizungumza wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani leo Alhamisi Mei 4,2023 katika ukumbi wa Lewis Kalinjuna.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imefanikiwa kuongeza kasi ya makusanyo ya mapato ya ndani ambapo kwa kipindi cha Julai mwaka 2022 hadi Aprili 30, 2023 imekusanya shilingi Bilioni 5 sawa na asilimia 108% ikiwa malengo ni kukusanya shilingi Bilioni 6 sawa na asilimia 140% ifikapo Juni 31,2023.


Hayo yamesemwa leo Alhamisi Mei 4,2023 na Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Jomaary Satura kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kilichokuwa na ajenda mbalimbali ikiwemo kupokea mihtasari ya kamati za kudumu kwa robo ya pili ya mwaka 2022/2023, kupokea taarifa za utekelezaji wa idara mbalimbali za kamati za kudumu kwa robo ya tatu 2022/2023 na taarifa kutoka kwa mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Jomaary Satura.

Mkurugenzi huyo wa Manispaa ya Shinyanga amesema  Julai 2022 hadi kufikia 30 Aprili 30,2023 mwenendo wa makusanyo ya mapato ya ndani umeimarika kwani wamekusanya asilimia 108% sawa na shilingi Bilioni 5.


“Matarajio yetu ifikapo Juni 31,2023 tutafikia lengo la makusanyo ya asilimia 140 sawa na shilingi bilioni 6 kama tulivyojiwekea malengo kwa mwaka 2023/2024 ili kuendelea kuwahudumia wananchi kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo”, amesema Satura.


Akizungumzia kuhusu mwenendo wa ujenzi wa miradi ya maendeleo, Satura amesema miradi inayoendelea kujengwa itakamilika haraka ili ianze kuwahudumia wananchi huku akiwaomba madiwani na wananchi waendelee kutoa ushirikiano ili miradi ikamilike vizuri.

“Miradi inaendelea vizuri hata ule ujenzi wa soko kuu Mjini Shinyanga na Ngokolo Mtumbani unaendelea vizuri na kwa weledi mkubwa na wafanyabiashara wana amani na matumaini makubwa juu ya miradi hii”,amesema Satura.
Kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga

“Tuendelee kuvumilia wakati miradi inaendelea kutekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa. Ni matumaini yetu pindi ujenzi utakapokamilika mauzo na mapato ya Halmashauri yataongezeka maradufu”,ameongeza Satura.

Katika hatua nyingine amewaomba Madiwani pindi panapotokea matatizo yanayoathiri wananchi kwenye maeneo yao, wasisubiri vikao vya Baraza la Madiwani bali wawasiliane na ofisi ya Mkurugenzi ili kutatua changamoto hizo haraka.


Kuhusu taarifa ya mifugo katika kata ya Mwamalili kufa kwa ugonjwa ambao haujafahamika, amesema ofisi yake imepokea taarifa hizo na inazifanyia kazi haraka iwezekanavyo na majibu yatapatikana haraka kwani mwananchi ni haki yake kuhudumiwa kwa viwango vinavyokidhi.
Naye Mchumi wa Manispaa ya Shinyanga Mensari Mrema amesema Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kwa kipindi cha robo ya tatu imepokea kiasi cha shilingi 1,715,900,000/= ikiwa ni fedha za bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya ujenzi wa matundu ya vyoo, ukamilishaji wa maboma ya madarasa, ujenzi wa vyumba vya walimu za 2 in 1 katika shule za msingi, ukarabati wa miundombinu katika shule za msingi tatu kongwe, ukamilishaji wa miundombinu ya bweni la wanafunzi na bwalo la chakula katika shule ya Sekondari Old Shinyanga.


Mbali na Mapokezi ya fedha za miradi ya maendeleo za mwaka 2022/2023 kutoka serikali kuu kwa kipindi cha robo ya tatu na nne kiasi cha shilingi 1,715,900,000/=,  Halmashauri pia imepokea fedha za kutekeleza miundombinu ya elimu msingi kupitia mradi wa Boost pamoja fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za viongozi ambao ni nyumba ya mkurugenzi na Mkuu wa Idara. 
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Mhe. Elias Ramadhani Masumbuko.

Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Shinyanga Elias Masumbuko amesema mafanikio makubwa yanayoonekana katika Manispaa ya Shinyanga yanatokana na ushirikiano mkubwa uliopo baina ya viongozi, wadau na wananchi.

“Tunamshukuru sana Mhe. Rais Samia kwa kuendelea kutupatia fedha kwa ajili ya maendeleo. Na sisi Shinyanga tuna kila sababu ya kumpongeza Mhe. Rais Samia kwa fedha anazoleta, Shinyanga inapiga hatua kimaendeleo. Waheshimiwa madiwani tuendelee kushirikiana katika kuhakikisha tunafanikisha miradi, tuna hofu ya Mungu hakuna atakayedokoa fedha za miradi”,amesema Masumbuko.

Meya huyo pia amewataka Madiwani kufanya mikutano ya hadhara kuhamasisha wananchi kuchangia chakula kwa ajili ya wanafunzi shuleni ili watoto wote wapate lishe shuleni.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Johari Samizi ameitaka Madiwani na Watumishi wa Halmashauri waendelee kuwa wabunifu katika ukusanyaji mapato na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Kila mmoja atimize wajibu wake katika kutekeleza miradi ya maendeleo. Sote tunatekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM na miongozo mbalimbali inayotolewa na serikali",amesema.


Aidha amehimiza ushirikiano katika kupambana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kuhakikisha binadamu wanabadili tabia zao kwa kutunza mazingira kwa kupanda miti na kutunza vyanzo vya maji kwani kuna baadhi ya watu wanaharibu kwa maksudi binafsi huku akisisitiza kuwa yeyote atakayeharibu vyanzo vya maji hatua za kisheria.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Johari Samizi akizungumza wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani.


Mkuu huyo pia amesisitiza wananchi kutumia mvua hizi za mwishoni zinazoendelea kunyesha kwa kupanda mazao ya muda mfupi na wataalamu wa kilimo wahakikishe wanatoa ushauri wa kitaalamu ili kuhakikisha wananchi wanatumia vizuri mvua hizi sambamba na kuhamasisha wananchi kutunza chakula.

Mkuu huyo wa wilaya amesema ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha anapiga suala la mmomonyoko wa maadili katika jamii na ukatili wa kijinsia.

“Tunasikia kuna ubakaji, ulawiti na usagaji. Tunasikia maneno yasiyo na mvuto kwenye masikio yetu. Ni jukumu letu kuhakikisha tunapiga vita mmomonyoko wa maadili na kupita vita matukio ya ukatili wa kijinsia”,amesema Mhe. Samizi.
Madiwani wakiwa kwenye kikao

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Andrew Kifua ameipongeza Manispaa ya Shinyanga kupata hati safi, utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na ukusanyaji wa mapato.


Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Mhe. Anord Makombe amesema ukusanyaji wa mapato katika Manispaa ya Shinyanga unaridhisha na kutokana na mambo mazuri na mageuzi makubwa yanayofanywa kwenye Manispaa hiyo maswali ya wananchi yanapungua kuhusu nini CCM imefanya katika jamii.


Wakichangia hoja mbalimbali, Madiwani wameomba miradi ya maendeleo kukamilishwa kwa wakati ikiwa ni pamoja na barabara za mitaa zilizofungwa zifunguliwe , wananchi kupatiwa huduma ya maji na umeme kwenye maeneo ambayo bado hayajafikiwa kutatua changamoto ya kukatika katika kwa umeme huku wakiipongeza serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo katika Manispaa ya Shinyanga.

ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Mhe. Elias Ramadhani Masumbuko akizungumza wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani leo Alhamisi Mei 4,2023 katika ukumbi wa Lewis Kalinjuna. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Jomaary Satura akizungumza wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani leo Alhamisi Mei 4,2023 katika ukumbi wa Lewis Kalinjuna.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Jomaary Satura akizungumza wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani leo Alhamisi Mei 4,2023 katika ukumbi wa Lewis Kalinjuna.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Johari Samizi akizungumza wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani leo Alhamisi Mei 4,2023 katika ukumbi wa Lewis Kalinjuna.
Kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kikiendelea
Mchumi wa Manispaa ya Shinyanga Mensari Mrema akizungumza wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Andrew Kifua akitoa salamu kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Mhe. Anord Makombe akitoa salamu kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Johari Samizi (kulia) akiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga. Kushoto ni Naibu Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Mhe. Esther Makune
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Johari Samizi (kulia) akiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.
Kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kikiendelea.
Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga wakiwa kwenye kikao
Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga wakiwa kwenye kikao
Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga wakiwa kwenye kikao
Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga wakiwa kwenye kikao
Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga wakiwa kwenye kikao
Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga wakiwa kwenye kikao
Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga wakiwa kwenye kikao
Viongozi wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini wakiwa kwenye kikao
Watumishi Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga na Taasisi mbalimbali wakiwa kwenye kikao

Wadau mbalimbali wakiwa kwenye kikao
Watumishi Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga na Taasisi mbalimbali wakiwa kwenye kikao
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages