Breaking

Saturday, 27 May 2023

DCEA, TAKUKURU KUIMARISHA USHIRIKIANO KUDHIBITI RUSHWA NA DAWA ZA KUELEVYA



************

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa wamesaini hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizi hususan katika kuzuia vitendo vya rushwa na dawa za kulevya hapa nchini kupitia vilabu vilivyopo katika shule za msingi , sekondari hadi vyuoni.

Makubalianao hayo yamesainiwa na Mkurugenzi wa TAKUKURU CP. Salum Hamduni na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo katika ofisi ya TAKUKURU makao makuu jijini Dodoma jana Mei 26, 2023. 

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari, CP. Salum Hamduni amesema, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupamban na Dawa za Kulevya na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa wamekubaliana kutumia rasilimali walizonazo kuwahamasisha wanafunzi, vijana na jamii kwa ujumla kutoshiriki vitendo vya rushwa na biashara haramu ya dawa za kulevya pamoja na kuchukua hatua stahiki za kukabiliana na mambo hayo.

‘‘Tuna matarajio makubwa baaada ya kusaini makubaliano haya kwani nguvu yetu ya kudhibiti dawa za kulevya na rushwa itaongezeka na kufanya jamii ya watanzania kuwa salama’’ amesema CP. Hamduni.

Aidha, amewaasa wanahabari kutumia vyombo vya habari kuunga mkono juhudi hizi kwa kuwahamasisha wananchi kushiriki katika kutokomeza vitendo vya rushwa na matumizi ya dawa za kulevya.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo amesema anafuraha kusaini MoU ambayo inawaunganisha TAKUKURU na DCEA katika kushirikiana kikazi kutoa elimu mashuleni na jamii kwa ujumla juu ya madhara ya dawa za kulevya na rushwa kwa jamii kwani makosa haya yanauhusiano wa karibu na yanahitaji suluhu ya pamoja.

Amesema, ‘‘muungano huu ni muhimu kwani utasaidia kufanya matumizi sahihi ya rasilimali chache tulizonazo kutatua matatizo mawili kwa pamoja’’

Pia amesema makosa yanayoshughulikiwa na Taasisi hizi mbili ni makosa ya kupangwa na vita dhidi ya makosa haya yanaupinzani kwenye jamii kwani yanaleta faida kwa wanayoyatekelezea hivyo kupitia ushirikiano huu na elimu itakayotolewa, vijana watajengewa hali ya uzalendo na kuijenga jamii kuchukia matendo ya rushwa na dawa za kulevya hivyo kuibua chachu ya maendeleo kwa Taifa.

Pamoja na hayo, kamishna jenerali Lyimo ameonesha nia ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kupingana na rushwa na dawa za kulevya kwa kusema, ‘‘Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ana dhamira ya dhati ya kuongoza jamii isiyo na rushwa wala dawa za kulevya, na kupitia makubaliano yaliyofanyika yataleta tija kwa jamii na kutimiza azma ya Mhe. Rais ya kuwa na jamii bora, ya wachapakazi, jamii ya wazalendo na jamii ya kulisukuma taifa mbele kupata maendeleo.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inaahidi kushirikiana kikamilifu katika kuisimamia na kuimarisha vita dhidi ya rushwa na dawa za kulevya, na tutaendelea kushirikiana kuhakikisha jamii inaelewa madhara ya Rushwa na Dawa za kulevya. Tumeamua kuwekeza nguvu kubwa katika kuzuia kuliko kukamata maana kukamata kunakuja pale ambapo nguvu ya kuzuia imeshindikana. amesema kamishna jenerali Lyimo.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages