Mbunge wa Viti Maalumu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Agness Hokororo (aliyesimama) akifungua mafunzo ya usalama na afya kwa wajasiriamali wa Mkoa wa Mtwara katika Wilaya ya Tandahimba yaliyowasilishwa na Meneja wa OSHA Kanda ya Kusini, Bw. Wilbert Ngowi (wa kwanza kushoto)
Mbunge wa Viti Maalumu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Agness Hokororo akizungumza na wajasiriamali wa Wilaya ya Tandahimba wakati wa mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi kwa wajasiriamali hao
Wajasiriamali wa Wilaya ya Tandahimba Mkoani Mtwara wakifuatilia mada ya masuala ya usalama na afya mahali pa kazi inayowasilishwa na Meneja wa OSHA Kanda ya Kusini, Bw. Wilbert Ngowi (mbele)
Meneja wa OSHA Kanda ya Kusini, Bw. Wilbert Ngowi (mbele) akifafanua kuhusu faida za kuzingatia masuala ya usalama na afya mahali pa kazi kwa wajasiriamali Mkoani Mtwara.
*******************
Na Mwandishi Wetu
Kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani yatakayofanyika Aprili 28, Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) wakishirikiana na Ofisi ya Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Mtwara wametoa mafunzo ya usalama na afya kwa wajasiriamali ziadi ya 300 Mkoani humo kwa lengo la kuwajengea uelewa wa kukabiliana na vihatarishi vya ajali na magonjwa katika maeneo yao ya kazi.
Akizungumza na wanahabari wakati akihitimisha mafunzo hayo ya siku tatu yaliyofanyika katika wilaya za Mtwara Mjini, Mikindani na Tandahimba, Mbunge wa Viti maalumu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Agness Hokororo amesema kuwa mafunzo hayo yatawaongezea tija wajasiriamali hao pamoja na kuwapunguzia gharama za uendeshaji wa maeneo yao ya kazi.
“Elimu hii ya masula ya usalama na afya itawaongezea tija wajasiriamali hawa kwa kiasi kikubwa sana pindi watakaporejea katika shughuli zao, pia itawaepusha dhidi ya ajali na magonjwa yanayoweza kuwakumba katika meneo yao ya kazi na kuwasababishia gharama kubwa za uendeshaji wa miradi yao hivyo basi niwasihi wajasiriamali wote waliopata mafunzo haya kuhakikisha wanazingatia ipasavyo miongozo ya usalama na afya waliyofundishwa kwani kutokufanya hivyo kunaweza kuathiri mlolongo mzima wa shughuli zao za uzalishaji” alisema Mhe. Agness Hokororo.
Kwa upande wake Meneja wa OSHA wa Kanda ya Kusini ambaye pia ni Mkufunzi wa Mafunzo hayo, Bw. Wilbert Ngowi amesema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya kampeni ya kuelekea katika maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yatakayo adhimishwa Aprili 28 Mwaka huu huku akiamini kuwa wajasiriamali hao wataitumia ipasavyo elimu hiyo katika kuboresha mifumo ya usalama na afya katika maeneo yao ya kazi.
“OSHA imeona ni vyema katika kipindi hiki tunachoelekea katika maadhimisho ya usalama na afya mahali pa kazi Duniani tuwe na mafunzo haya kwa wajasiriamali kwasababu nao ni sehemu ya uzalishaji mali na katika maeneo yao ya kufanyia kazi wanakumbana na vihatarishi vingi na wengi wao hawakuwa na uelewa mzuri juu ya namna sahihi ya kukabiliana na vihatarishi hivyo, tunaamini kuwa vikundi hivi vilivyonufanika na haya mafunzo vitakuwa chachu ya mabadiliko ya kiusalama katika maeneo mbalimbali ya kazi” alisema Bw. Ngowi.
Aidha Wajasiriamali hao kutoka vikundi mbalimbali Mkoani humo wanaeleza namna ambavyo elimu hiyo itawaletea manufaa katika shughuli zao za kila siku.
“Kabla ya kupata mafunzo haya tulikuwa hatujui namna sahihi ya kufanyakazi zetu kwa kuzingatia miongozo ya usalama na afya lakini sasa tumejifunza vitu vingi na kufahamu kuwa hata eneo kazi lisilofanyiwa usafi au lisilo na mpangilio mzuri wa vifaa linaweza kuwa chanzo cha ajali na magonjwa” alisema Bi.Eva Mhilu
Nae Bi.Rose Luhongo ambaye ni Mjasiriamali katika Wilaya Tandahimba amewasihi wajasiriamali wenzake kufanyakazi kwa tahadhari na kwa kuzingatia sheria na miongozo ya usalama na afya
“Tukifanya shughuli zetu kwa kuzingatia taratibu zote tulizoelekezwa kupitia mafunzo haya basi tunaweza kudumu na kuwa na nguvu kwa miaka mingi sana lakini tusipozijali afya zetu na kukiuka taratibu hizi basi tunaweza kupatwa na magonjwa au ajali zitakazotusababishia ulemavu ambao unaweza kukwamisha shughuli zetu za kiuchumi” alisema Bi. Rose.
Maadhimisho ya Kimataifa ya Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi hufanyika tarehe 26 hadi 28 mwezi Aprili kila mwaka na katika mwaka huu 2023 yanatarajiwa kufanyika Kitaifa Mkoani Morogoro katika Viwanja vya Tumbaku, Kauli mbiu ya maadhimisho ni ; Mazingira Salama na Afya ni Kanuni na Haki ya Msingi Mahali pa Kazi.