Breaking

Wednesday, 19 April 2023

TGNP-BAJETI YA TAMISEMI YA MWAKA WA FEDHA 2023-24 HAIKUANGALIA HEDHI SALAMA



NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

MTANDAO wa Jinsia Tanzania TGNP imeendesha Semina ya Jinsia na Maendeleo (GDSS) ambapo wamejadili Bajeti yenye mlengo wa Kijinsia na kuangalia ni nini sauti ya wananchi katika Bajeti ya 2023-2024 ya Ofisi ya Rais TAMISEMI.

Washiriki wa Semina ya jinsia na Maendeleo (GDSS) wametoa maoni yao kuhusu Bajeti ya TAMISEMI ya mwaka 2023-2024 na kuona haikuangalia hedhi salama ambapo hakuna fedha ambazo zilitengwa kwaajili ya kuongeza matundu ya vyoo katika shule zote hasa matundu ya vyoo vya wasichana, Maji mashuleni, maji kwenye zahanati na upatikanaji wa taullo za kike mashuleni.

Akizungumza katika Semina hiyo leo Aprili 19,2023 Jijini Dar es Salaam, Mwezeshaji na Mchambuzi wa Bajeti kwa Mtanzamo wa Kijinsia TGNP, Bw.Deogratius Temba amesema Bajeti ya mwaka huu ya TAMISEMI kumekuwa na ongezeko kubwa la fedha lakini hawakuona inakwenda kugusa moja kwa moja mahitaji ya wananchi.

Kwa upande wa Washiriki wa Semina hiyo wameomba Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kuendelea kuhamasisha jamii kushiriki kwenye Semina za Jinsia na Maendeleo ili kusaidia kufikia watu wengi zaidi na wao kushiriki katika shughuli za kimaendeleo kwenye maeneo yao.

Wamesema kupitia Semina hiyo inakwenda kuwajengea uelewa wao na jamii kwa ujumla katika kuweza kushiriki katika shughuli za kimaendeleo ikiwemo masuala ya Bajeti na ushirikishwaji wa wananchi katika kuandaa Bajeti na utekelezaji wake kama ilivyokusudiwa.

Mshiriki wa Semina hiyo, Bw.Mufat Mapunda amesema kuna uhaba wa uelewa wa masuala ya Bajeti kwenye jamii nzima hivyo kupitia semina ya leo ambayo ililenga kwenye mada ambayo iligusia masuala ya Bajeti wataenda kutoa elimu kwa jamii ili waweze kupata uelewa kuhusu masuala ya Bajeti.




















Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages