NA EMMANUEL MBATILO
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya kati imeteketeza bidhaa za chakula na vipodozi vilivyo chini ya kiwango kiasi cha Kilo 3509.09 zenye thamani ya Shilingi Milioni 33,677,685 ambapo ikijumuisha bidhaa za chakula ambazo ni Kilo 2098.727 zenye thamani ya Shilingi Milioni 11,943,835 na vipodozi Kilo 1410.303 zenye thamani ya Shilingi Milioni 21,733,850.
Akizungumza na waandishi wa habari katika zoezi hilo la kuteketeza leo Aprili 6,2023 Jijini Dodoma, Afisa udhibiti ubora Bw.Sileja Lushibika amesema bidhaa zote za chakula na vipodozi zilizoteketezwa ni zile bidhaa ambazo ziliisha muda wa matumizi, zenye viambata sumu na zile ambazo tarehe za mwisho wa matumizi zimekaribia.
Amesema bidhaa hizo zimepatikana kutoka kwenye maeneo ya biashara (maduka na maghala, Baa, hotelini na stoo zilizopo katika Halmashauri zote za Mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora ambazo zinaunda Kanda ya Kati kwa TBS.
Aidha amesema uwepo wa bidhaa zilizoisha muda wa matumizi na zile zenye viambato sumu zinaathiri uchumi wa nchi pamoja na afya za watumiaji.
"Bidhaa za chakula zilizoisha muda wa matumizi na zile ambazo tarehe za mwisho wa matumizi zimekaribia zinaathiri upatikanaji wa virutubisho vinavyotegemewa zinaweza kusababisha magonjwa ya muda mfupi na mrefu ikiwemo saratani". Amesema
Hata hivyo amesema upande wa vipodozi hasa vile vyenye viambato sumu, athari zake ni za muda mfupi na mrefu ikiwemo kuathiri ngozi, macho, mfumo wa uzazi kwa akina mama, ukuaji kwa watoto na magonjwa ya saratani hasa ngozi.
Pamoja na hayo ametoa wito kwa wafanyabiashara kukagua bidhaa zao mara kwa mara kujiridhisha na ubora wake, kutunza bidhaa hizo kwa mujibu wa taratibu za wazalishaji, kuepuka kuuza bidhaa za vipodozi zenye viambato sumu, kuacha mara moja kuhariri taarifa za mwisho wa matumizi na vilevile wazalishaji wa bidhaa kuthibitisha / kusajili bidhaa zao.