Breaking

Tuesday, 18 April 2023

RAIS SAMIA ALETA MAPINDUZI YA UCHUMI



* Tanzania kuchimba madini adimu ya kimkakati yanayosakwa dunia nzima kutengeneza vifaa nyeti vya jeshi, magari ya umeme 

* Serikali kuvuna mapato zaidi ya Shilingi trilioni 7.4 baada ya Rais Samia kuvutia wawekezaji wa nje kujenga migodi mikubwa mipya mitatu

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SERA za kuvutia wawekezaji za Rais Samia Suluhu Hassan na usimamizi madhubuti wa sekta ya madini zinatarajiwa kuiingizia serikali mapato ya zaidi ya dola za Kimarekani Bilioni 3.15 (zaidi ya Shilingi trilioni 7.4) kwenye miaka ijayo kufuatia kusainiwa kwa mikataba ya ujenzi wa migodi mikubwa mitatu kati ya serikali na wawekezaji wa nje.

Mikataba hiyo ya ubia ilisainiwa Jumatatu wiki hii jijini Dodoma kati ya Serikali na kampuni za uwekezaji za Australia na kushuhudiwa na Rais Samia.

Mkataba wa kwanza ni kati ya Kampuni ya Peak Rare Earths Ltd na Serikali ambapo wamekubaliana kuunda kampuni mbili za ubia za Mamba Minerals Corporation na Mamba Refinery Corporation. Serikali ya Tanzania itakuwa na umiliki wa asilimia 16 ya hisa katika kampuni hizo za ubia, wakati mwekezaji atamiliki asilimia 84.

Mradi huu utahusisha ujenzi wa mgodi wa madini adimu (rare earth minerals) wa Ngualla katika Mkoa wa Songwe, ambapo ujenzi unatarajiwa kuanza Oktoba mwaka huu na uuzaji nje wa madini hayo ya kimkakati umepangwa kuanza Septemba 2025 ili kujibu kiu kubwa iliyopo kwenye soko la dunia kwa madini hayo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Madini, mwekezaji anatarajiwa kutumia Dola za Kimarekani milioni 439 kwenye uwekezaji wa awali katika ujenzi wa mgodi huo na kutumia Dola za Kimarekani nyingine milioni 215 kuendesha mgodi huo.

Maoteo ya Wizara ya Madini yanaonesha kuwa mgodi huo utadumu kwa miaka 23 na kutengeneza mapato yafikayo Dola za Kimarekani Bilioni 6.8 wakati wa uhai wake.

Kati ya mapato hayo, Dola za Kimarekani Bilioni 2.37 (sawa na Shilingi trilioni 5.5) zinatarajiwa kwenda kwa Serikali ya Tanzania, ikitokana na hisa zake za asilimia 16 kwenye mgodi huo, mrabaha, tozo na kodi za moja kwa moja.

Nchi ya China inauza zaidi ya asilimia 80 ya madini ya rare earths duniani na kufanya nchi ya Marekani na Ulaya kusaka machimbo mengine ya madini hayo Tanzania na kwingineko, ili kupunguza utegemezi kwa China.

Madini hayo nyeti yanatumika kwenye ndege za kijeshi, magari ya umeme, vifaa vya kuzalisha umeme wa upepo na vifaa vya kielectroniki.

Kwa upande mwingine, Serikali imeingia ubia na kampuni ya Evolution Energy Minerals Limited ya Australia kujenga mgodi wa uchimbaji madini ya kinywe (graphite) eneo la Chilalo, Wilayani Ruangwa, Mkoa wa Lindi.

Kwenye mradi huu, jumla ya mapato ya serikali yanatarajiwa kuwa Dola za Kimarekani milioni 437 (zaidi ya shilingi trilioni 1) ndani ya miaka 18 ya uhai wa mgodi huo.

Mradi wa tatu unahusu ubia kati ya Serikali na mwekezaji kutoka Australia, EcoGraf Limited, utakaohusisha uchimbaji madini ya kinywe (graphite) kwenye eneo la Epanko, lilipo Mahenge, Wilayani Ulanga, Mkoa wa Morogoro.

Wizara ya Madini imesema kuwa Serikali inatarajia kupata mapato ya Dola za Kimarekani milioni 344.2 (zaidi ya shilingi bilioni 800) ndani ya miaka 17 ya uhai wa mgodi huo.

Serikali iko kwenye hatua za mwisho za majadiliano na kampuni nyingine za wawekezaji wa nje ambao wako tayari kujenga migodi mipya mikubwa minne mingine, hivyo kuzidi kupaisha uchumi wa taifa.

Licha ya mapato hayo ya serikali, wawekezaji hao wataingiza mitaji na ujuzi kutoka nje na kutengeneza maelfu ya ajira mpya.

Tangu alipoingia madarakani Machi 2021, Rais Samia amechukua hatua za makusudi kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini na kurejesha imani ya wawekezaji wa nje kwa nchi.

Takwimu mpya za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) zilizotoka wiki hii zinaonesha kuwa uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi tangu Rais Samia aingie madarakani, huku makusanyo ya kodi nayo yakivunja rekodi.

IMF imesema kuwa Pato la Taifa la Tanzania linatarajiwa kufikia Shilingi trilioni 200 mwaka huu kutoka Shilingi trilioni 163.5 wakati Rais Samia alipoingia madarakani mwaka 2021.

Takwimu hizo za IMF zinaonesha kuwa uchumi wa Tanzania utakua kwa kasi zaidi ya uchumi wa Kenya kwenye miaka mitano ijayo, hivyo kuipa uwezekano wa Tanzania kuipiku Kenya kwenye miaka ya karibuni na kuwa uchumi mkubwa zaidi kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

(MWISHO)
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages