Breaking

Sunday 16 April 2023

FISI WAVAMIA KIJIJI NGORONGORO, WAUA KONDOO 32




Kundi la fisi limevamia kijiji cha Njoroi kata ya Ololosokwani Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha na kuua kondoo 32.

Tukio hili limetokea Ijumaa Aprili 14, 2023  katika kijiji hicho kinachopakana na pori la akiba la Pololeti  na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Njoroi, James Memusi amesema fisi hao walivamia kijiji  saa tisa usiku na kuanza kushambulia kondoo na kuwaua 20 na kisha kuvamia makazi ya Mshao Tukai na kuua kondoo 12.


"Hili ni tukio la kwanza kutokea fisi kuvamia usiku na kula mifugo wengi kiasi hiki," amesema.

Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Jorome Mauri amesema, "kuna wanyama wengi porini kwa nini wamekuja huku kijijini? Tunaomba uchunguzi isije kuwa kuna kichaa cha fisi."

Hata hivyo mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (Tawiri), Dk Eblate Mjingo amesema hana taarifa kamili za tukio hilo.

"Kuna wataalamu wetu wapo huko tunafuatilia na tutatoa taarifa lakini yale maeneo yapo jirani ya  hifadhi hivyo inawezekana fisi kuvamia hayo maboma," amesema.


Chanzo: Mwananchi

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages