Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk.Franklin Rwezimula akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Abdul-Razaq Badru wakati Naibu Katibu Mkuu huyo alipotembelea HESLB jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Abdul-Razaq Badru (mwenye miwani) akizungumza wakati Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk.Franklin Rwezimula alipotembelea HESLB jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk.Franklin Rwezimula akipokea zawadi kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Abdul-Razaq Badru wakati Naibu Katibu Mkuu huyo alipotembelea HESLB jijini Dar es Salaam.
**********************
Na Mwandishi Wetu
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetakiwa kujiandaa kwa ongezeko kubwa la wanafunzi wahitaji wanaotokana na sera ya elimu ya msingi na sekondari bila ada ambao wanatarajia kujiunga na taasisi za elimu ya juu kuanzia mwaka 2026/2027.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Franklin Rwezimula amesema kuwa ni muhimu kwa HESLB kuwa na mipango inayoendana na mageuzi makubwa ya elimu yanayofanywa na Serikali ikiwemo kuwawezesha watoto kupata elimu ya msingi na sekondari bila malipo ya ada.
“Bajeti ya mikopo kwa mwaka huu wa 2022/2023 ni TZS 654 bilioni, na mwakani tutarajie itaongezeka zaidi … sasa ni vema mipango yenu (HESLB) iendane na ongezeko linalokuja kuanzia mwaka 2026/2027 ambapo matunda ya sera ya elimu bila ada yataanza kwenda elimu ya juu,” amesema Dkt. Rwezimula.
Dkt. Rwezimula ameyasema hayo alipokutana na Menejimenti ya HESLB katika ofisi za taasisi hiyo jijini Dar es salaam alipofika kujitambulisha na kubadilishana uzoefu baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 26 Februari mwaka huu.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru amesema Menejimenti ya HESLB imejipanga na kuandaa mapendekezo ya kuhimili ongezeko la wanafunzi wahitaji wa mikopo katika miaka ijayo.
“Hivi karibuni, tumefanya utafiti kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Uchumi (HEET) kuhusu matokeo ya elimu bila ada katika ugharimiaji wa elimu ya juu miaka ijayo … taarifa ipo na tutawasilisha kwa ajili ya ushauri na maandalizi,” amesema Badru.
HESLB ilianzishwa mwaka 2005 ikiwa na majukumu makuu mawili – kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji wa elimu ya juu na kukusanya fedha za mikopo zilizoiva zilizotolewa kwa wanafunzi tangu mwaka 1994/1995.