CEO Mugini (katikati), viongozi mbalimbali na vijana wakifurahia picha ya pamoja baada ya kukabidhi msaada wa mipira hiyo.
Na Mwandishi Wetu, Tarime
AFISA Mtendaji Mkuu (CEO) wa Mara Online, Mugini Jacob ametoa msaada wa mipira minane na kuikabidhi kwa vijiji vinne vya kata ya Nyanungu wilayani Tarime kwa ajili ya michezo kwa vijana.
Msaada huo uliombwa na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Nyanungu, Yakobo Kibiro baada ya kuona vijana katika vijiji hivyo ambavyo ni Kegonga, Nyandage, Mangucha na Nyamombara wanalazimika kutumia mipira iliyoshonwa viraka.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi mipira hiyo iliyofanyika kijijini Mangucha leo, Mugini amesema huo ni mwendelezo wa misaada ya kijamii anayoelekeza katika kata ya Nyanungu.
“Nimefurahi kufika hapa leo, nimefurahi kukutana na vijana wa Nyanungu, lakini zaidi nimefurahi kuwaletea zawadi ya mipira minane. Msaada huu unalenga kuelendeleza michezo kwa vijana wa kata hii,” amesema Mugini.
Mugini ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari amewahimiza vijana hao kusimamia ndoto zao na kutokubali kutumika.
Vijana hao na Katibu Kibiro wamemshukuru CEO huyo wa Mara Online ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Sauti ya Mara, na kumuomba kuendelea kuwasaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Katika tukio hilo, Mugini amefuatana na Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM Wilaya ya Tarime, Malema Solo ambaye amempongeza kwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu Sita chini ya Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza Ilani ya chama hicho tawala.
“Namshukuru Mkurugenzi wa Mara Online kwa kusaidia hawa vijana, msaada unaunga mkono utekelezaji wa Ilani ya CCM,” amesema Malema.
Mapema mwaka huu Mugini alipeleka msaada wa vitabu na mipira ya michezo kwa ajili ya wanafunzi wa kiume na kike katika Shule ya Sekondari Nyanungu.