Baadhi ya wahitimu wakipokea vyeti kutoka kwa mgeni rasmi
Baadhi ya wazazi wa wahitimu wakifuatilia matukio wakati wa mahafali hayo.
Wahitimu wa kidato cha sita wakitoa burudani wakati wa mahafali hayo.
Kampuni ya Barrick nchini imeeleza dhamira yake ya kuendelea kutoa fursa kwa Wanawake kufanya kazi kwenye migodi yake nchini ili kuondoa dhana iliyojengeka kwa muda mrefu kuwa ajira za migodini ni kwa ajili ya wanaume na imewataka wanafunzi walioko mashuleni na vyuoni kuchangamkia kusoma masomo yanayoendana na sekta ya madini kwa kujiamini.
Hayo yamebainishwa na Meneja Mawasiliano wa Barrick nchini, Georgia Mutagahywa , wakati wa mahafali ya kidato cha sita katika shule ya sekondari ya Jenerali David Musuguri, iliyoko Kata muhutwe wilayani Muleba Mkoani Kagera ambapo alikuwa ni mgeni rasmi.
Aliwaasa wahitimu hususani wasichana watakapojiunga na vyuo wasiogope kusoma masomo ya Jiorogia na mengine yanayohusiana na sekta ya madini kwa kuwa sekta hiyo bado inazo fursa nyingi na wanawake hawapaswi kuachwa nyuma kuchangamkia fursa hizo kama ilivyo sasa idadi ya wanawake ni wachache katika sekta ya madini kwa kulinganisha na Wanaume.
“Kampuni ya Barrick imedhamiria kwa dhati kuhakikisha inaongeza idadi ya wafanyakazi wanawake katika migodi yake ya Bulyanhulu na North Mara na hivi sasa tunao wafanyakazi Wanawake ambao wanaendelea kufanya kazi zao kwa ufanisi na weledi mkubwa”, alisema Mutagahywa.
Pia aliwataka wahitimu kutobweteka bali watumie elimu waliyoipata na watakayoendelea kuipata kuwa wabunifu ili watakaokosa ajira waweze kujiajiri na kutatua changamoto mbalimbali zilizopo kwenye jamii hususani kipindi hiki ambacho kuna upungufu mkubwa wa ajira nchini na katika nchi nyingi duniani kote.
Mkuu wa shule hiyo, Alchard Kashamba, alisema shule hiyo imefanya mahafali ya sita tangu, kupandishwa hadhi ya kuwa na kidato cha sita mwaka 2007 kwa kuongeza udahili wa masomo ya sayansi na Sanaa na kwa mwaka huu ikiwa na jumla ya wahitimu 264 wasichana.
Alisema kwa Sasa shule ina majengo 26 mabweni matano,bwalo la chakula Moja,maktaba na madarasa licha ya kuwa na changamoto ya baadhi ya vifaa vya kujifunzia na kufundishia kama wahitimu walivyoeleza katika risala yao kwa mgeni rasmi.
Mmoja wa wakazi wa kata ya Muhutwe Ansbert Mushumbushi, ambaye ni miongoni mwa wazazi waliohudhuria katika mahafali hayo alisema wanafurahishwa shule hiyo inavyoendelea kuwa na miundo mbinu mizuri na kufanya vizuri kitaaluma.