**********************
Wanafunzi wa kike wahandisi kutoka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) wamekuwa kivutio kwa wajasiriamali wanawake kwa bunifu zao zinazolenga kutatua changamoto kwa wajasiriamali.
Bunifu zilizooneshwa na wanafunzi hao ni mashine ya kubangua karanga pamoja na mashine ya kukunja vyuma vigumu ambavyo vinatumika kwa ajili ya madirisha ya nyumba na mapambo ya nyumbani.
Maonesho hayo yamefanyika leo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake duniani yaliyofanyika kwenye ofisi ya Mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa maonesho hayo Pili Kigome ambaye anafanya kazi za ujasiriamali amepongeza juhudi zilizofanywa katika kutengeneza mashine hizo ambazo zikipatikana sokoni zitawarahisishia kazi ambazo walikuwa wanaziogopa.
"Nimehamasishwa sana na hii mashine ya kukunja vyuma unajua kazi ya chuma inahitaji nguvu nyingi ambapo wakati mwingine wanawake wanaziogopa lakini tukipata mashine kama hii na sisi tutafanya maana hii ni kazi ambayo ukiifanya vizuri inalipa sana," amesema Pili.
Aidha, ameitaka DIT kuhakikisha kuwa mashine hizo zinakuwa sokoni na kwa bei nafuu kwa kuwa bado mtaji wao ni mdogo lakini mahitaji ya mashine hizi ni makubwa.
Katika maonesho hayo, mgeni rasmi Profesa Veridian Masanja ambaye ni mtaalamu wa masomo ya Hisabati kutoka Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela, amewataka wanafunzi hao kuboresha bunifu zao ili ziuzike ndani na nje ya nchi. Amesema kuwa bunifu zinahitajika kwenye jamii ili kutatua changamoto mbalimbali.
Maonesho hayo yamehudhiriwa na wanawake kutoka Mikoa ya Musoma, Kigoma, Shinyanga, Dodoma na Morogoro.