Na Selemani Msuya, Iringa
BODI ya Maji Bonde la Rufiji (RBWB) imesema ili kuhakikisha uwekezaji mkubwa wa miradi mbalimbali ya uzalishaji inakuwa endelevu wanatarajia kuajiri walinzi 50 ambao watalinda vyanzo mbalimbali vinavyotiririsha maji eneo hilo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa RBWB, Florence Mahay wakati akizungumza na waandishi wa habari kutoka katika vyombo vya habari mbalimbali ambao wapo kwenye ziara ya kutembelea bodi hiyo.
Mahay alisema bonde hilo linapokea maji kutoka mito mikubwa minne ambayo ni Ruaha Mkuu, Kilombero, Luwegu na Rufiji.
Mkurugenzi huyo amesema kutokana na faida ambazo zimeonekana na zinaendelea kuonekana wamejipanga kuongeza ulinzi kwenye bonde hilo ambapo katika mwaka wa bajeti wa 2023/2024 wanatarajia kuajiri walinzi 50 ambao watalinda vyanzo vilivyopo.
Amesema wamejipanga kulinda vyanzo vya maji vinavyoingiza maji katika bonde hilo, ili kuhakikisha shughuli za kiuchumi zilizopo zinakuwa endelevu, kwa kuwa zinachangia ukuaji wa uchumi.
Mahay amesema bodi hiyo ina kazi moja kuu ya usimamizi wa rasilimali za maji, kwa kuhakikisha wanatambua kiasi cha rasalimali maji kwenye bonde hilo, kugawa maji, kutunza vyanzo vya maji na kuzuia uchafuzi.
Mkurugenzi huyo amesema wamelazimika kuwapitisha waandishi wa habari katika maeneo ya Bonde la Rufiji, ili kuhakikisha umma unapata taarifa sahihi katika eneo hilo.
“Serikali imewekeza katika Bonde la Rufiji kwa kujuenga miradi ya kuzalisha umeme, kama Bwawa la Mtera, Kidatu na Kihansi na kwa sasa Mradi wa Uzalishaji Umeme wa Mwalimu Nyerere (JNHPP). Miradi yote hiyo ina mchango katika uchumi wa nchi kama unavyoona asilimia 80 ya umeme wa maji unatokea hapo.
Lakini pia ukubwa wa bonde hili unachangia asilimia 50 ya miradi kilimo cha umwagiliaji, kama chai na sukari, hivyo tunakuwa na usalama wa chakula na tuna mbuga za wanyama takribani sita,” amesema.
Mahay amesema kwa sasa Bonde la Rufiji lina maji ya kutosha ambapo kuna mita za ujazo bilioni 40, mita za ujazo bilioni 31 juu ya ardhi na bilioni 9 ni chini ya ardhi, huku maji yanatumika kwa kutolewa vibali ni mita za ujazo bilioni 2.4.
Amesema kwa sasa bodi hiyo imesitisha utoaji wa vibali vya maji ikiwa ni maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan, ili kuhakikisha maji yanajaa kwenye Bwawa la Nyerere ambalo linatarajiwa kuzalisha megawati 2,115.
Mahay amesema bodi hiyo haitasita kubomoa miundombinu ya wale ambao watabainika kutumia maji bila kupewa vibali, hivyo wataka wananchi hasa jumuiya za watumiaji maji kutoa taarifa pale wanapobaina.
“Naomba nisisitize kuwa bodi hii haitamvumilia mtu yoyote anashiriki kutumia maji bila kibali, jumuiya za watumia maji tunaziomba ziendelee kutoa ushirikiano, ili kuhakikisha uwekezaji unaofanywa na serikali unakuwa endelevu,” amesema.
Kwa upande wake Mhaidrolojia wa RBWD Ally Diwani, amesema kitengo chao kina vituo 137 ambapo vituo 59 vinapima maji juu ya ardhi, 29 chini ya ardhi na 49 vya hali ya hewa.
Amesema katika eneo hilo wana changamoto ya uharibifu wa vituo, wizi na uvunjaji wa vifaa vinasaidia kuchukua takwimu kwa ajili ya tathminj ya rasilimali maji kwenye bonde.
Naye Msimamizi wa Kitengo cha Ugawaji Rasilimali Maji wa Bodi, Mhandisi Gallus Ndunguru amesema hadi sasa wametoa vibali 2005 kwa watumiaji maji mbalimbali walioko katika eneo la bonde.
“Pia tumetoa vibali 10 vya kutiririsha maji taka kwa taasisi mbalimbali ambao wanatoa huduma zao kwa kutumia maji. Ila kwa sasa tumesitisha kutoa vibali vya wawekezaji wakubwa hasa katika maeneo ambayo yameathirika,” amesema.
Ofisa Maendeleo ya Jamii RBWB, Upendo Lugalla amesema katika kuhakikisha bonde hilo linakuwa endelevu wanataerajia kupata miti 200,000 rafiki na maji.
Amesema pia kupitia idara yao wamefanikiwa kuunda jumuiya 42 za watumiaji maji ambao wanashiriki kulinda vyanzo vya maji katika bonde hilo.
Mwisho