Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), James Shimbe ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Usimamizi TCB akizungumza na waandishi wa habari. Kushoto ni Afisa Kilimo Mwandamizi TCB, Renatus Luneja akifuatiwa na Mkaguzi wa Viuatilifu kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Richard Danstan. Kulia ni Mwenyekiti Msaidizi wa Kamati ya Kusimamia Usambazaji wa Viuadudu na Vinyunyizi vya zao la pamba, Bw. Protas Henry.
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Bodi ya Pamba Tanzania (Tanzania Cotton Board – TCB) imeeleza matokeo chanya ya mikakati ya kuongeza zao la Pamba katika kipindi cha miaka Miwili ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan huku ikiweka nguvu zaidi katika kutoa elimu kwa wakulima pamoja na kusimamia usambazaji wa viuadudu na vinyunyizi vya zao la pamba kuanzia kwenye maghala hadi kwa wakulima.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Alhamisi Machi 23,2023, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), James Shimbe ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Usimamizi TCB, amesema Bodi ya Pamba Tanzania inajivunia mafanikio makubwa ndani ya miaka miwili ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kikao hicho cha Bodi ya Pamba na Waandishi wa Habari Mjini Shinyanga kililenga kueleza mafanikio yaliyofikiwa na Bodi ya Pamba Tanzania ndani ya kipindi cha miaka miwili ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan sambamba na utekelezaji wa shughuli za kamati ya kusimamia usambazaji wa viuadudu na vinyunyizi vya zao la pamba kuanzia kwenye maghala hadi kwa wakulima ambayo iliundwa kutokana na agizo la Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe.
“Kwa kipindi hiki cha miaka miwili ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ambacho ametumikia wananchi vizuri na sisi tumefanya kwa juhudi kumuunga mkono na kuhakikisha kwamba wakulima wetu wanafanikiwa kama adhma ya serikali inavyotaka kwamba kuwe na maendeleo kwa wananchi/wakulima wenyewe na taifa kwa ujumla”, ameeleza Shimbe.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), James Shimbe ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Usimamizi TCB.
“Katika msimu huu wa kilimo 2022/2023 tuliagiza viuadudu chupa 11,839,225 zenye thamani ya shilingi Bilioni 51 ambapo lengo la kuagiza viuadudu hivyo ni kusambaza kwa wakulima kwa ajili ya kukabiliana na visumbufu vya zao la pamba. Hadi kufikia leo tumekwisha sambaza zaidi ya viuadudu chupa milioni 8”,amesema Shimbe.
Katika hatua nyingine amesema Msimu huu 2022/2023 zao la pamba linaenda vizuri sana na wanatarajia kupata mavuno ya pamba zaidi ya tani 500,000 (Kilo Milioni 500) huku akiongeza kuwa wanatarajia kuwa na ongezeko la pamba katika msimu 2023/2024 ambapo matarajio ni tani 700,000 kwa sababu hali ya hewa ni nzuri na bahati nzuri viuadudu vimepelekwa kwa wakulima.
“Lakini pia huwezi kupeleka viuadudu bila kuwa na vinyunyizi, tumenunua vinyunyizi 42,584 vyenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 4 na vyote tumevisambaza kwa wakulima na bahati nzuri vinafanya vizuri kwenye maeneo ya wakulima”,ameongeza Shimbe.
“Kabla ya vyote hivyo tumekwisha sambaza mbegu za kupanda za pamba ambazo zimeondolewa nyuzi kwa wakulima zaidi ya tani 22,000 kwa msimu huu 2022/2023. Bodi ya Pamba Tanzania imefanya hayo na inaendelea kusambaza viuadudu kwa wakulima”,amefafanua Shimbe.
Aidha amewataka wakulima kutambua kuwa bado viuadudu vipo na vinaendelea kusambazwa hivyo waendelee kujitokeza kwa wingi kunyunyizia mashamba yao ili wadudu wanaojitokeza wakiwemo funza, Chawa Jani, Vidukali na Vithrip (Thrips) waliopo kwenye mashamba waweze kuangamizwa ili kuhakikisha zao la pamba linaenda vizuri.
“Pamba inalimwa katika mikoa 17, Halmashauri 60 na halmashauri 56. Kwa sasa nchi nzima viuadudu vipo vinasambazwa na wananchi wakae mkao wa kuhakikisha mashamba yao yamekaa sawa kwa ajili ya kukabiliana na wadudu”,amesisitiza Shimbe.
James Shimbe
Katika hatua nyingine amesema TCB imenunua ndege 20 zisizo na rubani zenye thamani ya shilingi milioni 400 kwa ajili ya kunyunyizia viuadudu kwenye mashamba makubwa ya wananchi.
“Hali kadhalika Msimu huu tumejipanga vizuri kufikisha elimu kwa wananchi kilimo cha pamba, Balozi wa pamba nchini Aggrey Mwanri pia anaendelea kutoa elimu kwa wakulima. Tunawaomba wakulima wazingatie matumizi sahihi ya viuadudu lakini muda sahihi wa kunyunyizia”,amesema.
Ameongeza kuwa TCB pia imegawa baiskeli 2500 kwa wakulima wawezeshaji na pikipiki 250 kwa maafisa ugani ngazi ya kata katika halmashauri 13 ili kufikisha elimu kwa wakulima kuhusu kilimo cha pamba.
Richard Danstan akizungumza na waandishi wa habari
Kwa upande wake, Mkaguzi wa Viuatilifu kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Richard Danstan amesema viuadudu vinatolewa bure kwa wakulima na kwamba wanaendelea kufanya misako kwenye magulio na minada ili kuwabaini na kuwachukulia sheria wanaouza viuatilifu sambamba na kuhamasisha kuepuka kuweka viududu juani ili visipoteze ubora.
Renatus Luneja akizungumza na waandishi wa habari
Afisa Kilimo Mwandamizi Bodi ya Pamba Tanzania, Renatus Luneja amesema TCB inataka pembejeo zilindwe na ziwafikie walengwa huku akiwataka wakulima kufika katika AMCOS ili kuchukua pembejeo za kilimo badala ya kulalamika kuwa pembejeo zinachelewa kufika.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Kamati ya Kusimamia Usambazaji wa Viuadudu na Vinyunyizi vya zao la pamba inayoundwa na wajumbe 10, Mwenyekiti Msaidizi wa Kamati hiyo, Bw. Protas Henry amesema lengo la kamati hiyo ni kuhakikisha viududu na vinyunyizi vinawafikia wakulima.
“Kamati hii ina jukumu la kujiridhisha ubora na kiasi cha viuadudu kabla ya kusambazwa kwa wakulima, kuhakiki maelezo ya matumizi yaliyopo katika vifungashio kama yanaendana na yale yaliyoidhinishwa na mamlaka husika na kusimamia ugawaji wa viuadudu na vinyunyizi kwenye Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS),kufuatilia ufanisi wa viuadudu kwenye mashamba na kutoa ushauri wa kitaalamu”,ameeleza Henry.
Amesema kamati hiyo inaendelea kutekeleza majukumu yake tangu mwezi Desemba 2022 hadi sasa ambapo imekwisha fanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye AMCOS zinazohusika moja kwa moja na ugawaji viuadudu na vinyunyizi na kukutana na viongozi mbalimbali.
Mwenyekiti Msaidizi wa Kamati ya Kusimamia Usambazaji wa Viuadudu na Vinyunyizi vya zao la pamba, Bw. Protas Henry akitoa taarifa kuhusu shughuli za kamati hiyo.
“Miongoni mwa changamoto tulizobaini ni pamoja na viongozi wa kisiasa kama vile madiwani na wenyeviti wa vijiji/vitongoji kuingilia ugawaji wa viuadudu na vinyunyizi badala ya viongozi wa AMCOS, maafisa ugani na watendaji wa vijiji, baadhi ya viongozi wa AMCOS kutozingatia utaratibu wa ugawaji wa viuadudu na vinyunyizi na kujihusisha wizi wa pembejeo”, ameeleza Henry.
“Changamoto nyingine ni taarifa kwenye fomu za kugawia viuadudu na vinyunyizi kutojazwa kwa maksudi kwa nia ya kutengeneza mianya ya wizi wa pembejeo husika,baadhi ya viongozi wa AMCOS kughushi taarifa za kwenye fomu za kugawia viuadudu na baadhi ya wakulima kutoa taarifa zisizo sahihi za ukubwa wa mashamba yao ya pamba ukilinganisha na uhalisia”,amesema Henry.
Protas Henry akizungumza na waandishi wa habari
Kutokana na baadhi ya viongozi wa AMCOS kadhaa kuhusika katika tuhuma za wizi na kughushi taarifa za wakulima/viuadudu, Henry amesema jumla ya majalada 12 yamefunguliwa katika vituo vya Polisi, TAKUKURU kwa ajili ya uchunguzi katika wilaya za Bunda,Chato,Busega, Magu na Nyang’hwale na kamati hiyo imeokoa upotevu wa viuadudu vyenye thamani ya shilingi 34,370,000/=.
“Jumla ya kesi 6 zimefunguliwa mahakamani dhidi ya viongozi wa AMCOS kuhusu tuhuma za kupatikana na mali za serikali, wizi na kughushi katika wilaya ya Bunda, Chato, Igunga na Nyang’hwale lakini pia kesi moja imehukumiwa mahakamani ambapo mtuhumiwa alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja gerezani au kulipa faini ya shilingi 1,000,000/= katika wilaya ya Chato”,ameongeza Henry ambaye pia ni Mjumbe wa kamati ya kusimamia usambazaji wa viuadudu na vinyunyizi.
Henry amewakumbusha viongozi wa AMCOS na watendaji wengine waliopewa dhamana ya kusambaza na kugawa viuadudu na vinyunyizi kwa wakulima kutimiza wajibu wao kulingana na taratibu na sheria na kujiepusha na vitendo vya wizi, kughushi na rushwa kwa ajili ya kujipatia faida binafsi na kuwa tayari kuwafichua wote wanaohujumu usambazaji viuadudu na vinyunyizi ili hatua ziweze kuchukuliwa.
Mwenyekiti Msaidizi wa Kamati ya Kusimamia Usambazaji wa Viuadudu na Vinyunyizi vya zao la pamba, Bw. Protas Henry akitoa taarifa za utekelezaji wa shughuli za kamati hiyo leo Alhamisi Machi 23,2023.
Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog