Breaking

Tuesday, 7 March 2023

TBS YATOA ELIMU KWA WANANCHI MBEYA.


***********************

Shirika la Viwango nchini (TBS) limeendelea kutoa elimu kwa umma mkoani Mkoani Mbeya katika maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko kama masoko, vituo vya mabasi na viwandani lengo ni kuwajengea uwezo na utaratibu wa kupata alama ya ubora. 

Akitoa elimu kwa wafanyabiashara wa soko la SIDO Jijini Mbeya Afisa Masoko wa TBS Deborah Haule, amesema lengo la Shirika kutoa elimu hii ni kuwezesha wananchi kutambua shughuli zinazofanywa na TBS pamoja na kuwafikia wajasiriamali na wafanyabiashara mbalimbali ili wajue taratibu za kufuata katika huduma mbalimbali.

Deborah amesema kampeni yao hii watazifikia Halmashauri Wilaya za Mbeya Jiji, Chunya, Mbarali na Busokelo.

Aidha kwa upande wake Afisa Masoko wa TBS Mussa Luhombero, amesema elimu wanayoitoa ni bure na faida wanayoipata wajasiriamali ni pamoja na ushauri dhima ni kueneza uelewa na kukuza matumizi ya viwango na udhibiti ubora katika viwanda.

Baadhi ya wajasiriamali wa Soko la SIDO wamelipongeza Shirika la Viwango nchini kwa kutoa elimu na kwamba hawakuelewa kuwa huduma ya kuthibitisha ubora kwa wajasiriamali ni bure.

Stellah Mdem mfanyabiashara ya mafuta amesema elimu waliyoipata imewajengea uelewa mkubwa na kwamba sasa watauza bidhaa zenye ubora.

Naye Alestina Jestin amesema TBS itoe elimu mara kwa mara ili waendelee kupata elimu namna ya kutengeneza na kusambaza bidhaa zenye viwango.

Timu ya maafisa Masoko kutoka makao makuu itafanya kazi wiki mbili Mkoani Mbeya na kuhakikisha wananchi wamefikiwa na kupatiwa elimu hii ya viwango.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages