Breaking

Thursday, 23 March 2023

SERIKALI YASHAURIWA KUONGEZA BAJETI YA USIMAMIZI WA USALAMA NA AFYA NCHINI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako (aliyesimama) akimkaribisha Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi Khadija Mwenda (hayupo pichani) ili atoe mada kuhusu Muundo na Majukumu ya OSHA mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii katika Ukumbi wa Bunge Jijini Dodoma. Kulia kwake ni Naibu Waziri wake, Patrobas Katambi na kushoto kwake ni Katibu Mkuu wa Ofisi yake, Prof. Jamal Adam Katundu.


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii wakifuatilia mada kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda (hayupo pichani) aliyewasilisha mada inayohusu kuhusu Muundo na Majukumu ya OSHA.


Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda akiwasilisha mada kuhusu Muundo na Majukumu ya OSHA mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii.


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Fatuma Toufiq akiongoza majadiliano ya wajumbe wa Kamati hiyo mara baada ya Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda kuhitimisha mada aliyowasilisha katika kikao cha Kamati hiyo.


Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda akijibu hoja mbalimbali zilizoibuliwa na Wajumbe wa Kamati Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu masuala mbali mbali yanayohusu usalama na afya katika maeneo ya kazi nchini.


Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Athumani Maige, akiuliza swali kutokana na mada ya Muundo na Majukumu ya OSHA iliyowasilishwa na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, katika Kikao cha Kamati hiyo Bungeni jijini Dodoma.

************************

Na Mwandishi Wetu

Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeishauri serikali kuongeza bajeti ya usimamizi wa masuala ya usalama na afya ili kuuwezesha Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kuzuia ajali, magonjwa na uharibifu wa mali katika shughuli za uzalishaji hususan miradi mikubwa ya maendeleo jambo ambalo litaongeza kasi ya ukuaji wa uchumi nchini.

Ushauri huo umetolewa mara baada ya OSHA kuwasilisha randama ya bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 pamoja na taarifa ya muundo na majukumu yake mbele ya Kamati hiyo Bungeni Jijini Dodoma. Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii ndiyo inayoisimamia Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi chini yake ikiwemo OSHA kwasasa.

Akizungumza mara baada ya kuhitimisha kikao hicho, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Riziki Saidi Lulida, amesema OSHA ina jukumu kubwa la kusimamia mifumo ya kuzuia ajali na magonjwa katika maeneo ya kazi hivyo kupelekea shughuli za uchumi kufanyika kwa ufanisi mkubwa zaidi.

Kiongozi huyo wa Kamati ameongeza kuwa kutokana na jukumu hilo zito la OSHA, serikali haina budi kutenga bajeti ya kutosha ili kuiwezesha OSHA kufanya kazi yake ipasavyo hususan katika miradi mikubwa ya mafuta na gesi ambayo inahitaji kushughulikiwa kwa umakini mkubwa ili kuepuka madhara makubwa yanayoweza kutokea endapo ajali zitatokea katika maeneo husika.

“Uwepo wa OSHA ni mkakati wa maendeleo ya wafanyakazi na usalama wa nchi lakini watu wengi wanakwepa kutekeleza taratibu za usalama na afya kwenye maeneo ya kazi. Hivyo, sisi tunaishauri serikali isimame imara na iwape OSHA bajeti ya kutosha ili waweze kufanya kazi ya kuisaidia nchi katika eneo la usalama wa wafanyakazi katika viwanda vyetu, Taasisi zetu, mabomba yetu ya mafuta na gesi, mashirika ya umma na makampuni binafsi,” ameeleza Mbunge Lulida.

Aidha, Kamati hiyo imebainisha kwamba OSHA imeleta mabadiliko makubwa katika usimamizi wa masuala ya usalama na afya katika shughuli mbali mbali za uzalishaji mali ikiwemo sekta ya mafuta na gesi.

“Mafanikio ya OSHA ni makubwa sana endapo tukiangalia tulikotoka ambapo wafanyakazi walikuwa hawajui haki zao za msingi kuhusiana na masuala ya usalama na afya mahali pa kazi. Mathalani katika vituo vingi vya mafuta tulikuwa tunaona vijana wakitoa huduma bila kuzingatia matumizi sahihi ya vifaa kinga kama vile viatu maalum vya usalama (safety boots) badala yake walikuwa wanavaa ndala au lakini sasa hali imebadilika na vituo vingi wanazingatia taratibu muhimu za usalama na afya,” amesema Mariamu Kisangi, Mjumbe wa Kamati.

“Uwasilishaji wa leo wa OSHA umetufanya tuelewe kuwa Taasisi hii ina kazi kubwa sana, majukumu yake ni mazuri na inatekeleza majukumu yake kwa weledi na viwango vya hali ya juu. Taasisi hii inaishauri serikali vizuri kuhusiana na masuala ya usalama na afya na ni chombo ambacho waajiri na wafanyakazi wanakitegemea sana,” ameeleza Athumani Almas Maige ambaye ni Mjumbe Kamati.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema wamefarijika kuona kwamba wawakilishi hao wa wananchi wanatambua kazi kubwa inayofanywa na OSHA katika kusimamia uzingatiaji wa taratibu za usalama na afya kwenye maeneo ya kazi nchini.

OSHA ikiwa ni miongoni mwa Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu yenye jukumu la kusimamia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi, ilipata fursa ya kuwasilisha randama ya bajeti yake ya mwaka wa fedha ujao (2023/2024) pamoja na kueleza majukumu yake kwa Kamati hiyo ambayo ni mpya kwao kutoka Kamati ya Katiba na Sheria iliyokuwa ikiwasimamia hapo awali.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages