Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Songoro Mnyonge @mnyongesongoro amesema kampeni yake ya kutokomeza Madanguro haina lengo la kuwakomoa Madada wanaouza miili yao kwa kuwaacha wakihangaika bali amewataka wajisalimishe ofisi za Manispaa ili wapewe mikopo na mitaji ya kufanya biashara ili waache kujiuza.
“Mimi kabla ya kuwa Meya nilikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudhibiti UKIMWI ya Manispaa ya Kinondoni kwa miaka mitano mfululizo, nikiwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo tumekutana na Madada Poa wengi sana ambao tuliwaita na kuongea nao waache kujiuza wawe raia wema na wafanye kazi au biashara tulifanikiwa kwa kiwango kikubwa sana”
"Leo tuna mikopo ya asilimia 10, Mimi naita 442 (4% Wanawake, 4% Vijana, 2% Walemavu) tunatoa fedha mpaka sasa karibu Bilioni 18 zimezunguka kwa Wajasiriamali, Wiki mbili zilizopita tumetoa Bil 2.5, hawa Madada Poa ni Wanawake na Vijana"
"Wana nguvu na ari, kama ambavyo nimefika pale kwenye danguro wamekimbia ndani ya dakika mbili kumbe wanaweza kutumika kwenye ujasiriamali, tunataka wabadilike, tupo tayari kukaa nao kuwapa elimu na wabadilike, na tupo tayari kutafuta fedha maalum (Special Funds) kwa ajili yao ili ziwasaidie wapate mitaji, kama hoja ni mitaji tupo tayari na waking'ang'ania huko tutasema kuna jambo wanalitafuta"