MAKAMU wa Rais wa Marekani Mheshimiwa Kamala Harris anatarajiwa kutembelea Tanzania kuanzia tarehe 29 hadi 31 Machi 2023, kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Machi 14, 2023 na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Kwenye ziara hii ya kwanza nchini Tanzania na barani Afrika, Mheshimiwa Kamala Haris anatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mheshimiwa Haris na ujumbe wake pia watatembelea Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam na kukutana na vijana wajasiriamali wa Tanzania.
Pamoja na mambo mengine, ziara hii ya Mhe. Haris nchini Tanzania inalenga kuongeza nguvu katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Marekani na Tanzania hususan baada ya kufanyika kwa mkutano kati ya Marekani na nchi za Afrika maarufu kama US - Africa Summit mwezi Desemba 2022, ambapo Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alihudhuria.
Ziara hii ni ya kihistoria ambapo Makamu wa Rais wa Marekani ambaye ni mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo, anafanya ziara ya kikazi Tanzania na kukutana na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni Rais wa kwanza mwanamke wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ziara hii inafanyika takriban miezi 11 tangu viongozi hawa wawili wanawake walipokutana Ikulu ya Marekani na kubadilishana mawazo juu ya majukumu yao katika kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani uliodumu kwa miongo mingi tangu Tanzania ipate uhuru hadi sasa.
Aidha, ziara ya Mhe. Haris nchini Tanzania inalenga katika kuunganisha nguvu za ushirikiano wa kimaendeleo kati ya nchi Tanzania na Marekani katika sekta za afya, kilimo, utalii, uchukuzi, uchumi wa buluu, mawasiliano, uchumi wa kidijitali, uungaji mkono hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na uhimilivu wake na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kupitia ubunifu, ujasiriamali na uwezeshaji wanawake kiuchumi.
Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu ambazo Mhe. Haris na ujumbe wake watazitembelea ndani ya bara la Afrika kuanzia tarehe 25 Machi hadi tarehe 2 Aprili 2023. Nchi nyingine ni Ghana na Zambia.