Polisi nchini Peru wamemkamata msafirishaji wa bidhaa baada ya kupatikana na maiti ya kale katika begi lake.
Mwanamume huyo ambaye alikuwa akiisafirisha maiti hiyo na marafiki zake wawili, wakiwa walevi, walikamatwa na wanachunguzwa kwa uwezekano wa kutenda uhalifu dhidi ya urithi wa kitamaduni wa Peru.
Katika simulizi ya kustajabisha, mwanamume huyo alisema alikuwa akilala na maiti hiyo iliyokuwa imefungwa bendeji akiichukulia kama "aina ya bibi-harusi wa kiroho."
Huku akiipa maiti hiyo jina la "Juanita", alifichua kwamba ilikuwa mali ya baba yake, bila kutaja jinsi ilivyofika mikononi mwake
Kulingana na mwanamume huyo, alikuwa ameweka mabaki ya maiti hiyo kwenye begi ili kuwaonyesha marafiki zake.
Vyombo vya habari nchini humo viliripoti kuwa wataalamu waliohakiki uhalisi wa maiti hiyo ya kale walithibitisha kuwa ina umri wa kati ya miaka 600 na 800.
Vile vile walibaini kwamba maiti hiyo inalingana na mtu mzima wa kiume na wala sio wa kike kama mwanamume huyo alivyodai.