Breaking

Thursday, 16 March 2023

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII YARIDHISHWA NA TEKNOLOJIA YA MAWE KATIKA UJENZI WA BARABARA NGORONGORO


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeridhishwa na teknolojia ya tabaka gumu la mawe iliyotumika katika ujenzi wa Barabara ya Seneto hadi Kreta katika Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro. 

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mnzava(Mb) ametoa kauli hiyo leo wakati wa ziara ya kukagua mradi wa ujenzi wa barabara katika Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro Mkoani Arusha 

“Kwa kweli tumefurahishwa sana na aina hii ya teknolojia iliyotumika katika ujenzi wa barabara na sisi kama Kamati tutaendelea kuishauri Serikali kuitumia katika maeneo mengine yanayohitaji teknolojia ya aina hii” Mhe. Mnzava amesisitiza. 

Amefafanua kuwa awali barabara hiyo ilikua changamoto kwa watalii wanaoingia katika eneo la Kreta lakini kwa kazi iliyofanyika itaendelea kuwavutia wageni na kuhakikisha usalama wa wageni wanaotembelea Kreta ya Ngorongoro. 

Mhe. Mnzava ameipongeza Serikali kwa kutoa fedha zilizotumika katika ujenzi wa barabara hiyo na pia ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kwa kuisimamia kazi ya ujenzi. 

Ametoa wito kwa Serikali kuongeza juhudi na kasi katika kumalizia kipande cha barabara kilichobakia lakini pia kuangalia uwezekano wa kukarabati barabara nyingine za Ngorongoro ili kukuza utalii na kuongeza usalama wa watalii wanaotembelea eneo hilo. 

Naye, Naibu Waziri wa Maliasili nanUtalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amesema barabara hiyo ni hazina katika hifadhi kwa sababu imejengwa kwa kuokoa gharama ambapo awali zilipangwa kutumika kiasi cha shilingi bilioni 1.9 lakini imetumia kiasi cha shilingi bilioni 1.7. 

Amesema mfumo wa barabara za mawe ni bora zaidi kwa sababu ni rafiki wa uhifadhi na gharama nafuu ukilinganisha na barabara za lami. 

Ameongeza kuwa maelekezo yote ya Kamati ya kumalizia eneo la barabara lenye urefu wa kilomita 1.2 na kuangalia uwezekano wa kutumia teknolojia ya mawe katika maeneo mengine uhifadhi yatafanyiwa kazi. 

Ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara katika uhifadhi na uendelezaji wa utalii ambapo moja ya mikakati yake ni kuhakikisha miundombinu katika maeneo yote yaliyohifadhiwa iwe rafiki kwa watalii ili iwezeshe kuongeza idadi ya watalii.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages