Breaking

Monday, 6 February 2023

WATUHUMIWA WAWILI WAKAMATWA WAKITENGENEZA POMBE BANDIA


NA Mwandishi wetu Jeshi la Polisi

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limesema katika kuhakikisha linalinda raia na mali zao pia katika kuunga juhudi za serikali ya kuhakikisha raia wake wanakuwa salama kiafya tarehe 04.februari 2023 muda wa saa 11:00 jioni lilianza operesheni maalum ya kuwatafuta watu wote wanaojihusisha na utengenezaji wa pombe kwa kutumia nembo za makampuni yaliyosajiliwa.

Akitoa taarifa hiyo leo tarehe 06 februari 2023 kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha kamishina msadizi wa Polisi ACP JUSTINE MASEJO amesema Katika operesheni hiyo iliyohusisha vyombo vingine vya ulinzi na usalama huko katika kata ya Moivo, tarafa ya King’ori wilayani Arumeru walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili ambao ni Godfrend Brown (44) mfanyabiashara na mkazi wa Sanya Juu mkoani Kilimanjaro na Stive Haule (32) dereva wa lori na mkazi wa Moshi.

Kamanda Masejo amebainisha kuwa Mtuhumiwa Godfrend Brown alikamatwa akiwa na pombe za bandia boxi 154, vifaa mbalimbali vya kutengeneza pombe, stika za makampuni ya vinywaji mbalimbali na vifungashio vya pombe.

Aidha mtuhumiwa Stive Haule alikamatwa akiwa na gari aina ya Scania yenye namba za usajili T 191 CTB likiwa na tela lake lenye namba za usajili T 823 DHC tenka likiwa na ujazo wa lita 35,000 za spiriti.

Masejo aliendelea kufafanua kuwa gari hilo lilikamatwa muda wa saa 02:00 usiku huko maeneo ya King’ori katika wilaya ya Arumeru wakati likiwa linashusha mzigo wa spiriti kwa lengo la Kwenda kutengeneza pombe bandia.

Aidha Uchunguzi wa awali wa Jeshi hilo umebaini kuwa watuhumiwa hao wamekuwa wakijihusisha na vitendo hivyo vya kihalifu kwa muda mrefu. Aidha upelelezi ukikamilika jalada litapelekwa ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa ajili ya kulitolea uamuzi wa kisheria.

Sambamba na hilo kamanda Masejo amesema kuwa februari 02, 2023 muda saa 03:00 asubuhi huko katika Kijiji cha Kisimiri Juu Wilaya ya Arumeru Jeshi la Polisi mkoani hum lilifanya operesheni ambayo ilifanikisha kukamatwa kwa magunia 05 ya bhangi yenye uzito wa kilogramu 250 pamoja na kuteketeza hekari 07 za mashamba ya bhangi.

Jeshi la polisi mkoani humo limetoa wito kwa watu wachache wanaojihusisha na matukio ya uhalifu kuacha mara moja kwani wataendelea kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria kwa wote.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages