Watu 12 wamefariki dunia na wengine 63 wamejeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea usiku wa kuamkia leo Alhamisi Februari 9, 2023 wilayani Kongwa mkoani Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema kuwa ajali hiyo imehusisha magari mawili na kusababisha vifo vya watu 12 (wanaume 8, wanawake 4) na Majeruhi 63 (wanaume 40 wanawake 23).
Ajali hiyo imetokea usiku katika Kata ya Pandambili Kijiji cha Silwa wilayani Kongwa, barabara ya Dodoma - Morogoro.
Majeruhi wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Kongwa na Kituo cha Afya Gairo. Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mkoa wa Morogoro na majeruhi 2 wamehamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Ajali hii imetokea majira ya saa 6 usiku na imehusisha gari aina ya Lori lenye namba za usajili T 677 DVX na basi la abiri Kampuni ya Frester lenye namba za usajili T 415 DPP lililokuwa likitokea Bukoba kwenda Dar es Salaam
Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Kamishna Awadh Haji ametaja chanzo cha ajali hiyo kuwa ni mwendo kasi na uzembe wa dereva wa basi kutaka kulipita gari la mbele bila ya kuchukua tahadhari na kugongana na Lori lililokuwa limebeba saruji.
Akizungumza na wakazi wa Pandambili eneo la ajali Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ametoa rai kwa jamii kutii sheria bila shuruti ili kuepuka ajali.
"Serikali ilikuwa na nia njema ya kuruhusu vyombo vya usafiri kutembea usiku, lakini sasa baadhi ya madereva wanaanza kutozingatia Sheria za usalama barabarani, tutaendelea kuwachukulia hatua kali’’ Alisisitiza Mhe. Senyamule.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Dodoma amewatembelea majeruhi katika Hospitali ya Kongwa na Kituo cha Afya Gairo kutoa pole na kuwatakia uponyaji wa haraka.