Na Moshi Ndugulile, Shinyanga
Kaimu Mwenyekiti wa Halmashauri BAKWATA Mkoa wa Shinyanga Shekh Balilusa Khamis amesema ni wajibu wa viongozi wa Dini ya Kiislam kushirikiana na serikali pamoja na wadau wengine kuiombea Nchi na kuhamasisha amani.
Ametoa rai hiyo wakati akizungumza na viongozi wa kada mbalimbali za BAKWATA Wilaya ya Kishapu ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake, ambapo amewataka kuwa chachu ya kuhamasisha amani ya Nchi.
Shekh Balilusa amewakumbusha viongozi hao kuomba amani kwa ajili ya Nchi nyingine zinazokabiliwa na mizozo na vita ambapo waumini wake wamekuwa wakikosa nafasi ya kufanya ibada.
Kaimu Mwenyekiti huyo wa Halmashauri BAKWATA Mkoa wa Shinyanga amekumbusha pia wajibu wa viongozi wa Dini ya Kiislam kuwa kielelezo na mfano bora wa maadili mema ikiwa ni pamoja na kushirikiana na serikali katika jukumu la kusimamia maadili katika jamii.
Shekh Balilusa amesema wakati umefika kwa viongozi na waumini wa Dini hiyo kubadilika kulingana na mazingira yaliyopo kwa kuwatumia wataalam kutoka serikalini ili waweze kuwawezesha kuhusu namna bora ya kukuza uchumi kupitia biashara, kilimo na ufugaji.
Ziara ya Sheikh Balilusa ilitanguliwa na kikao cha ndani kilichofanyika Baina yake na Mkuu wa Wilaya ya kishapu Dc Joseph Mkude.
Katika kikao hicho Dc Mkude amesema serikali inatambua mchango wa viongozi wa dini katika kuchochea ustawi na maendeleo ya nchi, ambapo ameahidi kuendelea kushirikiana na taasisi za dini.