Na John Mapepele
Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (MNEC) wa Mkoa wa Pwani na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Mbunge wa Rufiji, Mhe. Mohamed Mchengerwa amemhakikishia Mlezi wa Mkoa huo, Makamu wa Rais, Mhe. Philipo Mpango kuwa wanakwenda kukijenga na kukiimarisha Chama ili kiweze kushinda kwa kishindo kwenye chaguzi zote zinazokuja.
Mhe.Mchengerwa ameyasema haya leo kwenye maadhimisho ya miaka 46 ya CCM, mjini Kibaha - Pwani wakati akitoa neno la shukrani kwa Mhe. Mpango.
Amesema wamepokea kwa maelekezo yote aliyoyatoa na wanakwenda kuyafanyia kazi mara moja ili kutatua changamoto za wananchi.
Aidha, amemhakikishia kuwa Chama kitashirikiana kikamilifu na Serikali ili kufanya kazi kwa pamoja na kuwaletea wananchi maendeleo.
Kuhusu kuwanoa wanachama ili waweze kuelewa Itikadi ya Chama amesema Mkoa utakwenda kutumia Chuo cha Uongozi cha Nyerere kilichopo mkoani hapo.
MNEC huyo na Mgeni Rasmi wamepanda miti ya kumbukumbu ya miaka 46 ya CCM katika shule ya Sekondari ya Tumbi na Chuo cha Uongozi cha Nyerere.
Katika hotuba yake, Mhe. Mpango amepongeza kazi nzuri inayofanywa na Chama.