Serikali imetumia kiasi cha shilingi milioni 710.7 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya utalii ya Pori la Akiba Pande ili kuhakikisha kuwa pori hilo linaendelea kuwa kitovu cha utalii katika jiji la Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb), ameyasema hayo leo Bungeni jijini Dodoma kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kibamba Mhe. Issa Mtemvu aliyetaka kujua mikakati ya Serikali ya kutumia Pori la Akiba Mabwepande kama chanzo cha mapato.
Amesema fedha hizo zimetumika katika ujenzi wa Kambi za Watalii mbili (2) katika eneo la Msakuzi na Jomeke na ujenzi wa maeneo mawili kwa ajili ya watalii kupumzika na kupata huduma mbalimbali (Picnic site) katika eneo la Bwawani na Crater pamoja na ujenzi wa uzio wa bustani ya wanyamapori kwa lengo la kukuza utalii katika eneo hilo.
“Ujenzi wa miradi ya miundombinu hiyo umekamilika na imeanza kutumiwa na watalii ambapo kwa sasa shughuli mbalimbali zikiwemo mbio za Marathon, nyama choma Festival, utalii wa kutembea kwa miguu na kuendesha baiskeli, upigaji picha na matamasha mbalimbali yamekuwa yakifanyika” Amefafanua Mhe. Masanja.
Akijibu swali la Mbunge wa Lupa Mhe. Masache Kasaka kuhusu Serikali kupunguza eneo la Msitu wa Mbiwe uliopo Chunya Mkoani Mbeya kwa ajili ya matumizi ya kiuchumi, Mhe. Masanja amesema Serikali haioni haja ya kupunguza eneo hilo kutokana na manufaa yake kwa Taifa.
“Hifadhi ya Msitu wa Mbiwe ni muhimu kwa kuhifadhi vyanzo vya maji; kuhifadhi mimea na wanyama; kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi; na kivutio cha utalii. Eneo hili pia ni ushoroba unaounganisha mapori ya akiba ya Rukwa - Lukwati, Lwafi na Hifadhi ya Taifa Katavi, hivyo kutonana na umuhimu huo Serikali haioni haja a kupunguza eneo hilo” amesisitiza Mhe. Masanja.
Msitu wa hifadhi wa Mbiwe una ukubwa kilomita za mraba 491 na umeanzishwa kwa Tangazo la Serikali Na. 598 la mwaka 1995.