Na Lucas Raphael,Tabora
NAIBU waziri wa ujenzi na uchukuzi mhandisi Godfrey Kasekenya amewaagiza mameneja ya wakala wa barabara nchini TANROADS kuhakikisha barabara zote nchini zinapitika ili kuwaondolea adha wananchi hasa katika kipindi cha mvua za masika .
Aliyasema hayo leo wakati akifungua mkutano wa 18 wa baraza la wafanyakazi wa wakala wa barabara TANROADS mkutano ulifanyika mkoani Tabora katika ukumbi wa Isike Mwanakiyungi.
Mhandisi Kasekenya alisema Kumekuwa na changamoto kubwa ya uharibifu wa miundombinu ya barabara hasa katika kipindi cha mvua masika na kuwafanya wananchi kushindwa kufanya shughuli mbalimbali za kujiletea maendeleo.
Alisema kwamba wananchi wamekuwa wakikabiliwa na adha kubwa ya kusafirisha bidhaa mbalimbali lakini pia hata kusafiri kufuata huduma za kijamii.
Hata hivyo naibu waziri huyo akikemea wizi wa alama za barabarani ambao umekuwa ukifanywa na baadhi ya wananchi wasio na nia njema .
Alisema kwamba hatua kali za kisheria zitaendelea kuchukuliwa kwa mtu,watu na kikundi chochote kitachobainika kufanya hujuma hizo za alama za barabarini.
Awali mtendaji mkuu wa TANROADS na mwenyekiti wa baraza Mhandisi Rogatus Mativila alibainisha kazi ambazo zimeendelea kufanywa na TANROADS kote nchini katika kuboresha miundombinu ya barabara.
Mhandisi huyo aliongeza kuwa kazi hizo ni pamoja na uwekaji wa alama za ukomo wa hifadhi za barabara ambapo hadi sasa zaidi ya kilometa 16,135 zimewekewa alama nchini.
Mhandisi Mativila wakala ya barabara inaendelea na utoaji wa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa kulinda miundombinu ya barabara.
Alisema baraza hili linafanyika mkoani Tabora likitanguliwa na mkutano wa 17 uliofanyika mwezi juni,2022 mkoani Mara kama unavyofahamu ambapo kufanyika kwa mkutano huu ni utekelezaji wa mkataba kati ya TANROADS na TAMICO pamoja na agizo la Rais namba 1 la majadiliano kati ya menejimenti nan a wafanyakazi.
Akitoa salamu za mkoa wa Tabora mkuu wa mkoa wa Tabora Balozi Dkt.Batilda Burian ametoa rai kwa wizara ya ujenzi na uchukuzi kukamilisha ujenzi wa barabara muhimu kwa uchumi wa mkoa.
Aidha mkuu huyo wa Mkoa alikiri kuwepo kwa changamoto ya wizi na uharibifu wa miundombinu ya barabara ambapo kuwa mkoa umeendelea na kukabiliana na hali sanjari na kushirikisha wananchi na viongozi wa vitongoji na vijiji.
Mwisho