Zaidi ya watu 20,000 sasa wamepoteza maisha katika tetemeko la ardhi la Jumatatu nchini Uturuki na Syria, ingawa Umoja wa Mataifa unaonya kwamba kiwango kamili cha maafa hayo bado hakijafahamika.
Waokoaji bado wanatafuta manusura kwenye vifusi, lakini matumaini yanafifia ikiwa ni karibu saa 100 tangu kutokea kwa tetemeko hilo.
Hali ya baridi kali inatishia maisha ya maelfu ya walionusurika ambao sasa hawana makazi, maji na chakula.
Rais wa Uturuki aliita tetemeko hilo "janga la karne".Juhudi kubwa za kimataifa za kutoa misaada zinaongezeka kwa kasi.
Siku ya Alhamisi Benki ya Dunia iliahidi msaada wa dola $1.78bn kwa Uturuki ikiwa ni pamoja na fedha za haraka kwa ajili ya kujenga upya miundombinu ya msingi na kusaidia wale walioathiriwa na tetemeko la ardhi.
Hapo jana maafisa walisema kuwa watu 17,600 wamekufa nchini Uturuki na idadi ya vifo ilikuwa angalau 3,377 nchini Syria.
Idadi hiyo inazidi ile ya zaidi ya 17,000 waliouawa wakati tetemeko kama hilo lilipotokea kaskazini-magharibi mwa Uturuki mwaka 1999.
Makumi ya maelfu ya watu kote Uturuki na Syria wanalala kwa usiku wa nne wakijikinga na halijoto kali katika makazi ya muda baada ya kukosa makazi kutokana na tetemeko hilo.