Mwanamke aitwaye Leah Nchimika(23)Mkazi wa Maganzo Wilaya ya Kishapu amefariki dunia baada ya kupigwa na shoti ya umeme akiwa anamuokoa mwanae Issa Saidi (02) asipigwe shoti ya umeme.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Majimaji Kata ya Maganzo Tarafa ya Mondo Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga,Sefa Ndekelo, amesema majira ya saa tatu asubuhi siku ya Jumamosi Febuari 4 mwaka huu alipewa taarifa kuwa mwanamke huyo amepata ajali ya umeme.
Amesema mwanamke huyo alikuwa akifanya jitihada za kumuokoa mwanae aliyekuwa amegusa waya (cable ya Runinga) na kueleza kuwa mama huyo alimuokoa mtoto bila kujua njia sahihi ya kufanya hali iliyosababisha kifo chake.
"Nilipata taarifa katika katika kitongoji changu kuna mwanamke amepata ajali akiwa anamuokoa mwanae aliyekuwa anaenda kwenye hatari ya kushika waya wa cable ya Runinga,mama mzazi akafika pale ili aweze kumuokoa mwanae yeye hakuelewa taratibu gani azifuate ili kuwa salama yeye na mtoto, alifika na kukamata waya na mtoto lakini alipigwa shoti na kuanguka na kupoteza fahamu,Polisi walifika pale wakamchukua na kumpeleka zahanati ya Maganzo na walivyofika hospitali wakaambiwa Leah amepoteza maisha", amesema Ndekelo.
Hata hivyo inaelezwa kuwa awali katika nyumba hiyo kulikuwa na tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shiyanga, ACP Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo halisi cha tukio hilo.
Via: Malunde 1 blog