Breaking

Thursday, 23 February 2023

WAZIRI KAIRUKI ATOA MAAGIZO SABA KWA WAGANGA WAKUU WA MIKOA NA HALMASHAURI



Na Angela Msimbira OR- TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Angellah Kairuki ametoa maagizo saba kwa waganga wakuu wa mikoa na Halmashauri ikiwemo kuwataka kufanya ukaguzi wa vifaa vya afya ili kudhibiti upotevu na matumizi mabaya ya bidhaa hizo.

Aidha, amewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri, waganga wakuu na wafawidhi wa vituo vya afya kuhakikisha fedha za Mfuko wa Afya wa pamoja zinatumika kwa wakati na kuzingatia mipango iliyoidhinishwa na hatakuwa na mzaha na watakaokiuka hilo.

Waziri Kairuki alitoa maagizo hayo leo Februari 22, 2023 jijini Dodoma wakati akifunga mkutano mkuu wa mwaka wa waganga wakuu wa mikoa na Halmashauri ambao uliambatana na uzinduzi wa mwongozo wa utekelezaji wa mshitiri kwenye ununuzi wa dawa,vitendanishi vifaa na vifaa tiba ili kudhibiti ununuzi holela wa bidhaa hizo.

Waziri Kairuki amesema kutofanyika kwa ukaguzi wa bidhaa za afya ikiwemo dawa, vitendanishi vifaa na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma za afya kunaweza kuchangia upotevu na matumizi mabaya ya bidhaa hizo.

“Nichukue nafasi hii kuwaelekeza Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kuwa kafanyeni ukaguzi wa vifaa vya afya kwa ushirikiano kati ya Idara ya Afya na Wakuu wa Idara nyingine ikiwa ni pamoja na wakaguzi wa ndani.

Pia kuanzia sasa ukaguzi wa bidhaa za afya itakuwa ni moja ya kiashiria cha ufanisi kwa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri,”alisisitiza Waziri Kairuki.

Amefafanua kuwa hilo litaenda sambamba na kuhakikusha kuwa vifaa tiba, mashine za maabara na X-ray zilizosambazwa katika vituo vya kutolea huduma za afya, Wahandisi wa vifaa tiba ngazi ya Halmashauri na watumiaji wa vifaa wanajengewa uwezo ili waweze kumudu kuvitumia na kuvifanyia ukarabati au matengenezo Kinga.

Waziri Kairuki amesema kilio cha kuchelewa kwa fedha za mfuko wa afya wa pamoja kimesikika na kwamba kutakuwepo utaratibu wa kutolewa mwanzoni mwa robo mwaka kama ilivyopendekezwa kupitia mkutano huo.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages