Breaking

Wednesday, 8 February 2023

HALMASHAURI ZATAKIWA KUTENGAFEDHA KUTEKELEZA MPANGO MATUMIZI YA ARDHI



OR - TAMISEMI

Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange(Mb) amesema Halmashauri za Wilaya zote nchini zimeelekezwa kutenga fedha kila mwaka katika bajeti zao kwa ajili ya kuandaa Mipango ya Matumizi ya Ardhi kwenye maeneo yote ya vijiji, pamoja na kuweka alama zinazoonekana kwa urahisi ili kuwezesha maeneo hayo kulindwa na kuzuia mwingiliano wa kimatumizi unaofanywa na wananchi.

Amesema hayo leo tarehe 08 Februari 2023 Bugeni Dodoma wakati akijibu Swali la Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini, Mhe. Francis Kumba Ndulane aliyetaka kujua Je, ni lini Serikali itatekeleza Mpango wa Matumizi bora ya Ardhi ili kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji katika Wilaya ya Kilwa?

Dkt. Dugange amesema ili kuondoa na kumaliza kabisa migogoro ya Wakulima na Wafugaji ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara, Serikali imejipanga kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji 6 kwa kila mwaka.

Aidha, Dkt. Dugange amesema Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa ina jumla ya vijiji 90 na kati ya vijiji hivi, vijiji 56 vina mpango wa matumizi Bora ya Ardhi mpaka kufikia mwaka wa fedha 2021/2022.

Amesema kwa mwaka huu wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga jumla ya Shilingi milioni 60 kwa ajili ya kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji vitatu vya Nandete, Kiranjeranje na Ruhatwe na kufanya urejeaji wa mipango ya matumizi ya ardhi iliyokwisha muda wake katika vijiji vitatu vya Kandawale, Likawage na Nanjilinji B.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages