Breaking

Sunday, 5 February 2023

DKT.MPANGO AWASIHI VIONGOZI CCM KUFANYA SIASA ZA KUJENGA TAIFA




Mjumbe wa Kamati kuu ya Halmshauri kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Mlezi wa CCM Mkoa wa Dar es salaam, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango amewasihi viongozi na wanachama wa CCM pamoja na Watanzania kwa ujumla kufanya siasa za kujenga taifa kwa kushindana kwa hoja na mawazo mbadala ya kujiletea maendeleo.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa Maadhimisho ya Miaka 46 ya Chama Cha Mapinduzi kwa Mkoa wa Dar es salaam yaliofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja leo tarehe 05 Februari 2023. Amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amejipambanua na kuonesha dhamira kwa vitendo ya kuweka mazingira mazuri ya demokrasia hapa nchini, upatanishi, kuvumiliana, kuishi pamoja na kujenga nchi hivyo ni vema kutumia nafasi hiyo kumuunga mkono kwa siasa safi zitakazo harakisha maendeleo.

Aidha Dkt. Mpango amewasisitiza viongozi wa Chama Cha Mapinduzi kutambua jukumu walilonalo katika taifa la kuwatetea wananchi, kusikiliza changamoto na kuzipatia ufumbuzi. Amewasihi viongozi wa Chama kuwa mstari wa mbele kuisimamia serikali katika utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020. Pia amewataka viongozi wa Chama kushirikiana na serikali katika kuhimiza wananchi kulipa kodi kwa maendeleo ya taifa.

Makamu wa Rais amesema serikali itaendelea kuboresha miundombinu katika Jiji la Dar es salaam ili kuondoa adha ya usafiri pamoja na kuchochea biashara na utalii katika mkoa huo. Amesema ujenzi wa Masoko Makubwa hususan katika Jiji Dar es Salaam, ikiwemo ukarabati wa Soko Kuu la Kariakoo ni dhamira ya serikali kuifanya Kariakoo kuwa kitovu kikubwa cha biashara kwa nchi zote za jirani.

Makamu wa Rais amesema Uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika na kuwa shindani huku mfumuko wa bei ukiendelea kuwa tulivu ambapo kwa mwaka 2022 ulikuwa asilimia 4.8, ndani ya malengo ya asilimia 3-5 ikiwa ni kiwango cha chini ukilinganisha na wastani wa asilimia 15.9 kwa nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Amos Makala amesema Soko la Kariakoo linatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu huku likiwatarajiwa kuwa na wafanyabishara 3500 kutoka wafanyabiashara wa awali 1200. Amesema kukamilika kwa soko hilo kutatoa fursa ya ufanyaji biashara kwa masaa 24 itakayochochea ukuaji wa uchumi wa Mkoa na Taifa kwa ujumla.

Makala amesema Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inaendelea kutekelezwa vema katika Mkoa wa Dar es salaam kwa uboreshaji wa sekta za Afya, Elimu, Miundombinu pamoja na Maji.

Awali aliyekuwa Mtia nia wa nafasi ya Urais kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dkt. Maryrose Majinge ameeleza katika mkutano huo uimara wa CCM katika kukabiliana na majanga yanapojitokeza pamoja na sera madhubuti zitakazowaleta wananchi maendeleo.

Amesema kuwa Maendeleo ya kweli hayapatikani kwa kukipa lawama chama tawala na kuibua hisia kwa wananchi kwa kuhesabu miaka ya tangu taifa kupata uhuru bali kila mtanzania anapaswa kubadili Imani na mtazamo wake na kuwajibika ipasavyo kuleta maendeleo kwa pamoja.

Katika Maadhimisho ya Miaka 46 ya Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Dar es salaam Jumla ya wanachama wapya 580 wamejiunga na Chama hicho akiwemo aliyekuwa Mtia nia wa nafasi ya Urais kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dkt. Maryrose Majinge.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages