Wamiliki wa Vituo Binafsi vya kutolea Huduma za Afya wametakiwa kuhakikisha wanazingatia utoaji wa huduma bora za Afya Kwa mujibu wa Kanuni na Miongozo ya Serikali.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Dr. Rashid Mfaume ametoa maelekezo hayo wakati wa kikao kazi na Wamiliki wa Vituo Binafsi vya kutolea huduma Afya kwenye Mkoa huo.
Aidha Dr. Mfaume amesema Vituo Binafsi vimekuwa na mchango Mkubwa katika kusaidia utoaji wa huduma Bora za Afya ambapo takwimu zinaonyesha Mkoa huo una zaidi ya Vituo Binafsi 800 sawa na asilimia 85 ikijumuisha Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali ambapo upande wa Serikali Kuna Vituo zaidi ya 170.
Pamoja na hayo Dr. Mfaume ametoa wito kwa Wamiliki hao kuhakikisha wanaajiri Madaktari, Wauguzi na Wataalamu wa Maabara wenye Sifa na weledi na sio kuajiri watumishi wasio na Sifa.
Miongoni mwa changamoto zilizobainika kwenye baadhi ya Vituo Binafsi ni pamoja na Upatikanaji wa taarifa ambapo Dr. Mfaume amewaelekeza kuwa wepesi wa kutoa taarifa kwa mujibu wa taratibu na Miongozo.
Kuhusu suala la Mavazi ya heshima, Dr. Mfaume amewataka watumishi wa afya kuhakikisha wanavaa sare zinazokubalika huku akikemea uvaaji wa Vikuku, Kope bandia, Nywele ndefu na sare zisizokubalika.