Mkuu wa wilaya Mbinga, Aziza Mangosongo amewatunuku vyeti wahitimu 17 wa mafunzo ya elimu ya teknolojia stahiki ya nguvu kazi (ukandarasi) na kugawa kadi za matibabu kwa uongozi wa chama cha walemavu.
Kozi ya ukandarasi imetolewa na wakufunzi wawili kutoka chuo cha teknolojia ya ujenzi Mbeya (Institute of Construction Technology ICoT--Mbeya), Chuo ambacho kipo chini ya wizara ya ujenzi na uchukuzi.
Hafla hii ya ugawaji vyeti imefanyika katika ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Mbinga Februari 03, 2023.
DC Aziza amewashukuru wakufunzi Eng.Richard Kansimba na Donatha Kamwela kwa kufika na kutoa mafunzo yenye tija kwa vikundi hivyo huku akiwashukuru wadau kwa kutambua umuhimu wa kusaidia vijana kwa ufadhili wa kutoa gharama za mafunzo ili kuwezesha kupata mafunzo yatakayosaidia kupunguza tatizo, kwa vijana wengi kujiajiri na kuongeza kipato.
Amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri ya Mbinga Mji na Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kupitia kwa maafisa maendeleo jamii kutumia asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri kuvipatia vikundi hivo mikopo ili vikafanye kazi kutokana na mafunzo ambayo wameyapata ili viweze kujiajiri na kuajiri vijana wengine ili kupunguza changamoto ya ajira, kujikwamua kiuchumi na kuongeza kipato.
Aidha, amewataka TARURA na TANROADS Mkoa wa Ruvuma kuwapatia kazi vijana hao ili wakatimize ndoto na mafunzo waliyopatiwa ili kuleta uhalisi katika utekelezaji wa majukumu Mbalimbali huku akiwataka wahitimu hao kufanya kazi kwa kufuata sheria na taratibu zilizopo pamoja na kuchangamkia fursa zinapojitokeza.
DC. Aziza alikabidhi kadi za matibabu 63 kwa viongozi wa chama cha walemavu ili idadi ya Walemavu ambao hawakupata kadi awamu ya kwanza wakapatiwe ili kuweka mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu kupata matibabu.
Akitoa taarifa kuhusu hali ya utoaji wa elimu ya mafunzo hayo, Eng. Donatha Kamwela amefafanua kuwa idadi ya washiriki ilikuwa ni 17 kutoka katika vikundi 3 kutoka katika Halmashauri ya Mbinga mji na halmashauri ya wilaya ya Mbinga.
"kozi ililenga katika utangulizi wa teknolojia stahiki ya nguvu kazi, upimaji wa barabara, teknolojia ya udongo, teknolojia ya zege, usajili wa vikundi, utunzaji wa kalvati na usimamizi wa mikataba, Kozi hii ilikuwa ni ya mwezi 1" ameeleza Eng.Donatha
Kwa upande wao wahitimu wa mafunzo ya elimu ya teknolojia stahiki ya nguvu kazi walitumia nafasi hiyo kumshukuru Mkuu wa Wilaya ya Mbinga kwa maono makubwa na juhudi za kuwaunganisha wadau mbalimbali akiwemo Mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi ya Ovans, Meneja Tanroads Mkoa, Meneja Tarura Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kwa kuatmbua umuhimu wa vikundi hivyo kupata mafunzo, ambapo wadau hao walitoa jumla ya tshs milioni 10, gharama ya kufanikisha mafunzo hayo.