Breaking

Saturday, 4 February 2023

AJALI YAUA WATU 17 TANGA, RAIS SAMIA AOMBOLEZA



RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameeleza kusikitishwa na ajali iliyoua watu 17 mkoani Tanga.

Hayo ameyabainisha leo Februari 4,2023 kupitia taarifa fupi aliyoitoa katika kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii.

"Nimesikitishwa na vifo vya watu 17 vilivyosababishwa na ajali iliyotokea jana saa 4:30 usiku eneo la Magila Gereza, Wilaya ya Korogwe, Mkoa wa Tanga.

"Nawapa pole wafiwa na wote walioguswa na vifo hivi. Nawaombea ndugu zetu hawa wapumzike mahali pema na majeruhi wapone haraka,"amesisitiza Rais Dkt.Samia

Katika taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omary Mgumba leo imeeleza kuwa ajali hiyo imehusisha magari mawili na kusababisha vifo vya watu 17 na Majeruhi 12.

Ajali hiyo imetokea usiku katika eneo la Magira Gereza Kata ya Magira Gereza Tarafa ya Mombo wilayani Korogwe, barabara ya Segera - Buiko.

"Ajali hii imesababisha vifo 17 na majeruhi 12 ambao majina yao wote hayajafahamika, miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali yetu ya Wilaya ya Korogwe na majeruhi 10 wamehamishiwa Hospitali ya Mkoa wa Tanga, Bombo na majeruhi wawili wamebaki Hospitali ya Korogwe kwa matibabu.

“Ajali hii imehusisha gari aina ya Mitsubishi Fuso na Coaster iliyokuwa imebeba mwili wa marehemu na abiria 26 ikitokea Dar kwenda Moshi kwenye mazishi” imeeleza taarifa hiyo.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages