Breaking

Thursday, 23 February 2023

WATUMISHI WA UMMA WATAKIWA KUWAHUDUMIA VIZURI WANANCHI




Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewaasa watumishi wa umma nchini kuwahudumia vizuri wananchi ambao ndio walengwa wakuu wa huduma zitolewazo na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Ndejembi wito huo kwa watumishi wa umma, wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Mji Njombe mkoani Njombe kilicholenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao katika halmashauri hiyo.

Mhe. Ndejembi amesema, kila mtumishi wa umma nchini akitimiza wajibu wake kuna uwezekano mkubwa wa kutatua matatizo ya wananchi kwani kila mtumishi wa umma kwa nafasi yake ni mwakilishi wa Serikali hivyo anapaswa kuilinda taswira ya Serikali kwa kutoa huduma nzuri kwa wananchi ili wananchi wajivunie uwepo wa serikali yao.

Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, watumishi wa umma wanapaswa kutoa huduma bora kwa wananchi kwani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesimamia na anaendelea kusimamia vema masilahi ya watumishi wote wa umma nchini, hivyo ni wajibu wa kila mtumishi kufanya kazi kwa bidii ikiwa ni sehemu ya kuthamini na kuunga mkono jitihada hizo za Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa Upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Njombe, Mhe. Erasto Mpete amemshukuru Naibu Waziri Ndejembi kwa kufanya ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Mji Njombe ili kuhimiza uwajibikaji, kusikiliza na kutatua kero za watumishi wa halmashauri hiyo kitendo ambacho kimejenga ari na morali ya utendaji kazi wa watumishi wa umma katika halmashauri yake.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi anaendelea na ziara yake ya kikazi katika Halmashauri ya Mji Njombe kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma, kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma ikiwa ni pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Halmashauri hiyo ya mji mkoani Njombe.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages