Mkuu wa Wilaya Mbinga Aziza Mangosongo amewaasa Madiwani kusimamia vizuri miradi ya maendeleo inayotokana na fedha zinazotolewa na serikali kuu na halmashauri.
Ameyasema hayo katika kikao cha robo ya pili ya mwaka 2022_2023 cha baraza la madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kujadili kilichokaa kujadili mikakati, mipango na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya serikali.
Dc Aziza Alimtaka Mwenyekiti wa Halmashauri na Mkurugenzi kuiruhusu kamati ya fedha kukagua miradi mara kwa mara kabla ya viongozi wengine kupita kukagua miradi hiyo na kuwaagiza Madiwani kuainisha Miundombinu iliyoharibika katika maeneo yao na taarifa hizo ziwasilishwe TARURA ili Fedha za dharura zitumike kutatua changamoto hizo.
Pia alimtaka Mkurugenzi kuhakikisha mipango ya ujenzi wa mabweni katika shule ya sekondari Mndeme na Ruanda iratibiwe kutokana na shule hizo kuzungukwa na migodi, hivyo ni rahisi watoto hasa wakike kingia katika hatari ya kupata mimba.
Vilevile alieleza juu ya usimamizi madhubuti wa rukuzu ya pembejeo za kilimo ili kuondoa kero za upatikanaji na ulanguzi wa bei kubwa kinyume na maagizo ya serikali, jambo linalo pelekea uwepo wa malalamiko mengi.
Aidha, DC Aziza alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo miradi ya vyumba vya madarasa, vituo vya afya, Zahanati, Maji Miundombinu na huduma zingine muhimu.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Haule na Mkurugenzi Mtendaji Mhe. Juma Haji walisema wamepokea maagizo hayo na utekelezaji wake utaanza haraka sana ili kuendana na kasi ya serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo, Vilevile walimshukuru Mhe.Mangosongo kwa kuhudhuria kikao hicho muhimu.