Breaking

Thursday, 16 February 2023

MOTO WATEKETEZA BWENI SHULE YA SEKONDARI LUGARAWA NJOMBE



NA MWANDISHI WETU

WANAFUNZI 82 wa Shule ya Sekondari Lugarawa wilayani Ludewa mkoani Njombe wamenusurika kuungua baada ya bweni lao kuteketea kwa moto na kuunguza mali za wanafunzi na za shule zenye thamani zaidi ya shilingi milioni 18.

Akizungumza kuhusiana na tukio hilo mkuu wa shule hiyo Everine Somola, amesema kuwa,tukio hilo limetokea majira ya saa tatu usiku wa kuamkia leo wakati wanafunzi wakiwa kwenye masomo ya usiku.

“Bweni hili wanaishi wanafunzi 82 ambao ni wavulana na wakati moto unatokea hakukuwa na mwanafunzi bwenini kwani ilikuwa ni muda wa masomo ya usiku hivyo walikuwa darasani,” amesema.

Hata hivyo ameongeza kuwa uongozi wa shule hiyo huwa wana utaratibu wa kila baada ya saa moja wanafunzi wawili huzungukia mabweni kuangalia usalama hivyo muda huo wanafunzi walipita na kuona moto huo ukiwaka kwenye ‘Main switch’ huku moshi ukiwa umetanda eneo lote.

Amesema kuwa chanzo cha moto huo kinahisiwa ni hitilafu ya umeme hivyo umeteketeza vitu mbalimbali ikiwemo vitanda, magodoro na baadhi ya vifaa vingine vya wanafunzi ambavyo kwa ujumla pamoja na jengo vimekadiliwa kuwa na thamani ya zaidi shilingi milioni18.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Castory Kibasa amesema tayari hatua za awali zimeanza kuchukuliwa kwa kununua magodoro na vitu vingine lakini bado wanahitaji msaada zaidi kutoka kwa wadau mbalimbali ili kuhakikisha mazingira ya wanafunzi hao yanarejea katika hali ya kawaida.

Sanjari na hilo pia amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Ludewa Joseph Kamonga kwa kuonesha ushiriki wa haraka ambapo baada ya kupata taarifa ametoa kiasi cha shilingi Milioni moja na kuahidi kufika eneo la tukio.

Deogratias Massawe ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ludewa amewataka walimu na viongozi wa shule zenye mabweni kuhakikisha wanafuata utaratibu wa ulinzi waliofundishwa na askari ambao wamekuwa wakipita shuleni kwa lengo la kutoa elimu mbalimbali za usalama.

“Tumekuwa tukipita katika shule mbalimbali na hasa ambazo wanafunzi wanaishi hapo, na kuwapa elimu juu ya ulinzi shirikishi ambapo muda wa masomo ya usiku wanatakiwa kuwepo bwenini wanafunzi watano kwa ajili ya kulinda usalama pia viwepo vifaa vya kuzimia moto kama ndoo zilizojazwa mchanga,” amesema.


Via:DiraMakini
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages