Breaking

Saturday, 7 January 2023

WAZIRI MKUU ATOA MAAGIZO KWA VIONGOZI WA HALMASHAURI




WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa Halmashauri zote nchini waweke mpango wa namna bora ya kuviwezesha vikundi vya wajasiriamali katika maeneo yao kupitia mikopo ya asilimia 10 ya makusanyo ya ndani ambayo itawawezesha kuendeleza miradi yao na kuleta tija.

“Badala ya kutoa mikopo ya fedha kidogo kidogo mnaweza kutoa fedha nyingi kwenye kikundi kimoja kimoja kama shilingi milioni 200 kukiwezesha kikundi husika kuanzisha mradi mkubwa ambao unaweza kuwaingizia fedha nyingi hivyo kuongeza tija”

Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amemtaka Meneja wa TARURA mkoa wa Ruvuma ashirikiane na Meneja wa TARURA wa wilaya ya Mbinga kufanya tathimini ya mahitaji ya matengenezo ya mtandao wa barabara katika maeneo ya uchimbaji wa makaa ya mawe na kuhakikisha zinapitika wakati wote ili kuwawezesha wawekezaji kufanya shughuli zao kwa ufanisi.

Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Januari 7, 2023) baada ya kutembelea na kukagua shughuli za uchimbaji wa makaa ya mawe katika mgodi wa kampuni ya Jitegemee Holdings ulioko katika kijiji cha Mdunduwalo, Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma.

Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji hivyo ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) lihakikishe linafikisha umeme wa gridi ya Taifa katika migodi ya makaa ya mawe mkoani Ruvuma ili kuwapunguzia wawekezaji gharama za uendeshaji.

Akizungumza baada ya kutembelea kampuni ya makaa ya mawe ya Jitegemee holdings, Waziri Mkuu amezitaka Jumuiya za Chama cha Mapinduzi wilaya ya Mbinga kuwekeza katika utengenezaji wa nishati ya mkaa wa kupikia kwa kutumia makaa ya mawe ili kudhibiti ukataji wa misitu na kuhamasisha utunzaji wa mazingira.

Kampuni hiyo imefanikiwa kuchangia shilingi bilioni 7.01 katika pato la Taifa, kati yake shilingi milioni 81.73 zimelipwa kwa halmashauri kupitia tozo na ushuru mbalimbali na Shilingi Milioni 292 ni kodi nyingine za serikali ikiwemo PAYE, kodi ya zuio na SDL.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages