Breaking

Friday, 20 January 2023

WAZIRI KAIRUKI AKEMEA TABIA ZA WATUMISHI KUTOA RUSHWA KUPATA NAFASI ZA UONGOZI


Na Angela Msimbira, MWANZA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Angellah Kairuki amekemea vikali tabia ya baadhi ya watumishi kutoa rushwa ili kupanda madaraja na kupandishwa vyeo.

Waziri Kairuki ametoa karipio hilo wakati wa kufungua kikao kazi cha mapitio ya tathmini ya utekelezaji wa shughuli za uboreshaji elimu nchini kilichofanyika jijini Mwanza,

Amesema kutoa rushwa kwa ajili ya kupata teuzi, kupanda madaraja na vyeo suala sio suala jema na halina nafasi.

Aidha, Waziri Kairuki ametoa rai kwa watumishi kuacha tabia ya kutoa rushwa ikiwa sifa, weledi, uzoefu na vigezo anavyo amewataka kujiamini kwa kuwa nafasi zipo

“Watumishi wenzangu kama vigezo vyote unavyo kama uzoefu, weledi, sifa kwa nini udanganyike kutoa chochote ili upate nafasi? kama nafasi ipo, ipo tu, kama mwenyezi Mungu amekuandikia utaipata usidanganywe na mtu,” amesisitiza Waziri Kairuki
Amesema amewatahadharisha watumishi waliopata vyeo kwa kutoa rushwa kuwa Serikali kwa sasa imeanza utaratibu wa kupitia upya daraja la kila mtumishi ili kujua aliingia kwa sifa zipi, vigezo vipi na kama bado anastahili kuendelea kuwa katika nafasi aliyonayo sasa.

Kairuki amesema kuwa kwa wale ambao wana vigezo amewataka kuhakikisha wanaendelea kusimamia sifa za utendaji wa utumishi wa umma na uadilifu, wasidanganyike kupita njia fupi kwa kutegemea mtu yeyote atakusaidia ili uweze kufikia nafasi ya uongozi.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages