Breaking

Saturday, 14 January 2023

WATU SITA WAKAMATWA TUHUMA ZA KUMUUA MWALIMU WA SHULE YA MSINGI AKIDAIWA KUCHEPUKA


Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi linawashikilia watu sita kwa tuhuma za kumuua mwalimu wa Shule ya Msingi Ugalla Wilaya ya Mpanda na kisha kumtupa mtoni baada ya kumfumania akifanya mapenzi na mke wa mtuhumiwa mwenzao.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi Ally Hamad Makame amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Sud Athuman , Sangalo Said , Mrisho Hamis ,Juma Kanyama Malim Anton na Taus Hamis wote wakazi wa Kijiji cha Ugalla Wilaya ya Mpanda .

Ameeleza kuwa watuhumiwa hao wote sita walikamatwa mnamo Januari 9 mwaka huu majira ya saa nane usiku huko katika eneo la Kijiji cha Ugalla .

Kamanda Ally Hamad Makame ameeleza kuwa mnamo tarehe 28 mwezi wa 12 mwaka 2022 huko katika mto Ugalla zilipokelewa taarifa kuwa kuna mwili wa mtu umeonekana unaelea ndani ya maji ya mto ugalla ambaye hakuweza kufahamika kwa jina wala sura baada ya kuwa mwili huo umeharibika vibaya .

Baada ya mwili huo kuwa umeopolewa ndani ya maji uchunguzi ulifanyika wa kidaktari na ndipo ulipoonesha kuwa mwili huo ulikuwa na majeraha ya kupigwa na uliweza kutambuliwa kuwa ni mwili wa mwalimu wa Shule ya Msingi Ugalla baada ya uchunguzi huo wa daktari msako ulianza wa kuwabaini watu waliofanya mauaji hayo.

Kufuatia msako huo mkali uliofanywa na jeshi la polisi ndipo mnamo tarehe 9 polisi walipofanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao wote sita .

Kamanda Makame amebainisha kuwa katika uchunguzi wa awali umebaini kuwa marehemu kabla ya kuuawa alifumaniwa na mke wa mtu ndipo watuhumiwa hao waliamua kumpiga na kumtupia mtoni .

Watuhumiwa wote wanaendelea kushikiliwa na Polisi na mara baada ya upelelezi kukamilika watafikishwa Mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Via: Malunde 1 Blog
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages