Breaking

Thursday, 5 January 2023

WASIMAMIZI ELIMU WATAKIWA KUJITATHMINI UFUATILIAJI MWENENDO WA ELIMU



Asila Twaha, TAMISEMI

Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Elimu Dkt. Charles Msonde amewataka viongozi wanaosimamia elimu katika Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa kujitathmini katika ufuatiliaji wa mwenendo wa elimu kwa watoto kwa kujua kusoma,kuandika na kuhesabu wanaomaliza elimu ya msingi.

Dkt. Msonde ameeleza hayo tarehe 4 Januari, 2023 katika Kikao kazi cha Maafisa Elimu wa Mikoa, Wilaya, Taaluma na Watu Wazima kilichofanyika Dodoma.

Amesema kutokana na tabia ya baadhi ya viongozi kusahau majukumu yao kwa kutowafuatilia walimu sehemu zao za kazi na kushindwa kufanya kazi kwa waledi, inapelekea kutokuwepo kwa ufanisi katika kazi na matokeo yake kusababisha kutopatikana kwa elimu bora na watoto kumaliza elimu ya msingi kushindwa kusoma, kuhesabu na kuandika.

Aidha, amewataka viongozi hao kutokubali kukabidhiwa watoto kuanzia darasa la awali kutoka kwa wazazi/walezi na kisha mtoto huyo amalize darasa la saba kwa kutokujua kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK).

“Hilo halitakubalika baadhi ya watu waharibu mipango na malengo ya Serikali, haiwezekani mtoto anamaliza darasa la saba hawezi kusoma, kuhesabu na kuandika ingelikuwa ni mtoto wako kama mzazi utajisikiaje kama kiongozi uliyepewa dhamana ikitokea hivyo maanake jitathmini hutoshi” amesisitiza Dkt. Msonde

Amewataka viongozi hao kutojikweza kwa uongozi na madaraka sababu sio lengo la Serikali bali lengo ni kwenda kushirikiana na walimu kwa kuwafuatilia na kujua changamoto kwa pamoja na kuzipatia ufumbuzi na sio kuwakatisha tamaa walimu.

Dkt. Msonde amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kujenga na kuboresha elimu nchini pamoja na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia Januari, 2023 watoto wengi wataingia shule fedha zilizotolewa za ujenzi wa madarasa 8000 asilimia 96 yamekamilika tushirikiane na jamii ili watoto hao waliochaguliwa waingie shuleni.

“Tuna walimu wazuri wakihamasishwa kwa kupewa motisha, ari na hamasa ya kufanya kazi tutakuwa na taifa bora sababu wataalamu wetu wengi wanatokana na walimu ” Dkt. Msonde

Kwa upande wake Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) Bi. Paulina Nkwama amewataka viongozi hao kusimamia misingi ya utumishi wa walimu katika kuwafuatilia maadili na utekelezwaji wa majukumu yao ikiwemo suala la ufuatiliaji wa utoro wa walimu ambao unazorotesha elimu na kama walimu watakuwa vizuri kwa kutekeleza kwa ufanisi, waledi na ubunifu tutakuwa na watu wenye elimu bora nchini.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Elimu Ofisi ya Rais- TAMISEMI Bw. Vicent Kayombo ametoa rai kwa viongozi hao kwenda kuyasimamia na kuyatekeleza maelekezo waliyopangiwa na viongozi hao sababu wameaminiwa na ni jukumu lao kusema wanaenda kuleta mabadiliko ya elimu kwa maslahi ya taifa.

Katika hatua nyingine, Dkt. Msonde amewataka viongozi hao kusimamia kwa kuwaandaa watoto kuanzia darasa la Awali ili wanapofika darasa la nne na saba wafanye vizuri zaidi na sio kuwaacha mpaka wafike madarasa hayo ndio watumie nguvu kubwa.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages