Na. Asila Twaha, TAMISEMI
Mkurugenzi wa Sera na Mipango Ofisi ya Rais TAMISEMI Bw. John Cheyo amesema Serikali imeanza kufanya tathmini ya vyanzo vya mapato kwenye Halmashauri zote nchini ili kubaini fursa zilizopo katika ukusanyaji wa mapato na kuweka mikakati ya kukusanya mapato kitaalamu na sio kwa mazoea ili kuongeza mapato hayo.
Bw. Cheyo ameyasema hayo Januari 05, 2023 wakati kikao cha tathmini ya mapato kwa Halmashauri za Mkoa wa Dodoma kinachoendelea kwenye shule ya Sekondari ya Dodoma.
Amesema ili Halmashauri iwe Halmashauri lazima mapato na hakuna Halmashauri bila mapato na kwa kipindi kirefu Halmashauri nyingi zinakusanya mapato kwa mazoea ndio maana tumeona tufanye tathmini hii mapema kwa pamoja kuangalia fursa zilizopo katika kila Halmashauri na kuweka Bajeti ambayo ni halisia kutokana na takwimu za vyanzo vya mapato.
Ameongeza kuwa ili Mkurugenzi awe bora anatakiwa awe na sifa ya ukusanyaji mapato na ili Halmashauri iweze kufanya matumizi inatakiwa kukusanya kwanza hivyo tunajipanga katika eneo hili ili huko mbeleni tuweze kuongeza mapato mara dufu kwenye Halmashauri zetu nchini.
Halkadhalika alibainisha kwamba ukusanyaji wa mapato unategemea takwimu sahihi hivyo kwa tathmini hii tutapitia chanzo kwa chanzo na kukijadili kwa kina kwa pamoja tujiridhishe kuwa hapa tumetafakari vya kutosha na kiwango cha ukusanyaji kilichowekwa ni halisi na kinaakisi takwimu zilizopo.
“Kuna mazoea yaliyojengeka katika kuandaa bajeti hasa kwenye mapato ya ndani ya Halmashauri unaweza kuta Halmashauri imepanga kukusanya shilingi mil 100 kutoka chanzo cha leseni za biashara lakini ukichunguza kwa kina hawana takwimu sahihi ya wafanyabiashara waliyopo katika Halmashauri zao huenda wamekaridia wale wa mjini tu au wale wakubwa lakini wafanya biashara wapo wengi na kiwango walichoweka kinaweza kuongezeka endapo kitafanyiwa tathmini ya kina.
Kupitia zoezi hili tunataka kuongeza bajeti ya makusanyo ya ndani ya Halmashauri zetu kwenye Bejeti inayokuja ya 2023/24 ili Halmashauri ziweze kutekeleza miradi ya maendeleo na shughuli zingine zote za Halmashauri husika bila vikwazo vya fedha.
Akizungumza katika kiko hicho Meneja wa Mamalaka ya Mapato Tanzania kwa Halmashauri za Wilaya ya Chemba na Kondoa Bw. Mohammed Kapera amesema zoezi hilo litatoa fursa ya kuendelea kuongeza idadi ya walipa kodi na kwa ushirikiano wa TRA na Halmashauri ukusanyaji wa mapato ya Serikali utaongezeka.
Naye Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu Mkoa wa Dodoma Bw. Charles Mduma amesema zoezi hili litasaidia Halmashauri za Mkoa wa Dodoma kupanga na kupata makisio halisi ya bajeti zao kwa mwaka 2023/24.
Aidha, amesema hapo awali Halmashauri hupanga makisio ya ukusanyaji ambayo sio halisi na kupelekea baadhi ya Halmashauri kuomba kuongezewa vifungu vya bajeti hali hiyo inadhihirisha wazi kuwa wakati wa kuandaa bajeti tathmini ya vyanzo vya mapato haikufanyika kikamilifu.
Zoezi hili litaendelea katika Halmashauri zote nchini kuanzia tarehe 09/01/2022 na linashirikisha wataalam wa Ofisi ya Rais –TAMISEMI, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wizara ya Fedha na Mipango, Sekretarieti za Mikoa na baadhi ya wataalamu kutoka Halmashauri zote nchini.