OR -TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais -T AMISEMI anayesimamia Elimu, Dkt. Charles Msonde amesema katika mwaka wa fedha 2022/23, Serikali inatarajia kujenga shule mpya za sekondari za kata 184 huku kila halmashauri ikipata shule moja.
Shule hizi zinajengwa kupitia awamu ya pili ya utekelezaji wa Mpango wa Uboreshaji wa Elimu ya Sekodari (SEQUIP).
Dkt. Msonde ameeleza hayo Januari 6, 2023 wakati wa ziara ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa katika Halmashauri ya Namtumbo Mkoani Ruvuma ya kukagua shule maalum ya wasichana ya Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Kupitia Mradi wa Kuboreshaji wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) katika mwaka wa fedha 2021/22 tayari zimejengwa shule 232 za kata na mwaka huu wa fedha kabla ya kufika mwezi Juni 2023, tutakuwa tumekamilisha ujenzi wa shule mpya 184 za kata, na kiÅ‚a halmashauri itapata shule moja," amesema Dkt. Msonde.
Dkt. Msonde ameeleza kuwa ujenzi wa shule za sekondari za kata utaenda sambamba na ujenzi wa shule mpya 5 nyingine za wasichana za sayansi zinazopaswa kujengwa kila Mkoa.
Awamu ya kwanza ya ujenzi wa shule za wasichana za sayansi ilihusisha ujenzi wa shule 10 ambazo ziko katika hatua mbalimbali za ukamilishaji kwa gharama ya Sh. bilioni 30.
Aidha, Dkt. Msonde amefafanua katika ujenzi wa shule za sekondari za kata utagharimu Sh milioni 600 kwa kila shule lakini awamu ya kwanza ya ujenzi Serikali inatoa Sh. milioni 470 kwa kila shule na Sh. milioni 130 zitatolewa katika awamu ya pili ambazo zinatumika kujenga nyumba za walimu na kununua vifaa vya TEHAMA vya kujifunzia.
Wakati huo huo, amewatoa hofu wazazi kwa kueleza kuwa Serikali imeweka jitihada kubwa ya kuboresha shule zote za kata kwa kuboresha miundombinu ili kuwapunguzia wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata elimu ya sekondari kwa kujenga Shule ya Sekondari kila kata.