Na John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Serikali inakwenda kuimarisha sekta ya Michezo na Sanaa ili kuinua uchumi na kusaidia uboreshaji sekta nyingine zote hapa nchini.
Akizungumza katika uzinduzi wa mashindano ya Kombe la Gwajima( Gwajima Super CUP) linaloratibiwa na Mbunge wa Kawe, Josephat Gwajima leo, Januari 1, 2023 Waziri mchengerwa amesema kuwa endapo sekta hizo zikiimarishwa zitakuwa chachu na nguzo ya kuboresha sekta zote.
Amesema mageuzi na mapinduzi makubwa yanayofanyika kwenye sekta hizi ni maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Amesema Mhe, Rais amekuwa na maono makubwa ndiyo maana ameunda Wizara mahususi ya Utamaduni Sanaa na Michezo ambayo ni nguvu shawishi katika Taifa.
Amesisitiza kuwa maono yake ni kama maono aliyokuwa nayo Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliyejenga miundombinu ya michezo katika kipindi chake.
Amesema dhamira ya Serikali kwa sasa kwenye michezo ni kuendelea kuwekeza katika miundombinu ambapo amesema kutakuwa na ukarabati wa miundombinu ya michezo kwa shule 56.
Ameongeza kuwa viwanja vikubwa saba vya michezo vinakwenda kukarabati na kujenga kiwanja cha kisasa katika jiji la Dodoma.
Aidha, amesema ukarabati huo ni mkakati wa makusudi wa Serikali wa kutaka kuwa wenyeji wa mashindano ya AFCON.
Pia, amesema kuimarika kwa sekta hizo kutatengeneza ajira nyingi na kuwa na mabilionea wengi ikiwa ni pamoja na kuwa na wachezaji wa bora wa taifa.
Aidha, amesema Serikali inatarajia kujenga uwanja changamani wa kisasa ( sports arena) jijini Dar es Salaam katika eneo la Kawe utakaochukua zaidi ya watu 16,000.
Amempongeza Mhe. Gwajima kuanzisha mashindano hayo na kutoa wito kwa wadau wengine wa michezo kuandaa mashindano kama hayo ambapo amesema kwa kufanya hivyo wana wanatekeleza Ilani ya CCM.