Breaking

Thursday, 26 January 2023

RAIS SAMIA ASISITIZA UWEZESHWAJI WA VIJANA KUPITIA UMILIKI WA ARDHI



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imetenga hadi eka 10 kwa kila kijana mwenye sifa ambapo baadae watazimiliki.

Kupitia taarifa iliyotolewa leo Januari 26, 2023 na Mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais ikulu Zuhura Yunus imeeleza kuwa Rais Samia amesema Tanzania iko katika mchakato wa kupokea maombi kwa kundi la kwanza la vijana watakaopata fursa ya kupata mafunzo ya miezi mitatu kuanzia katikati ya mwezi Februari halafu wagaiwe ardhi.

Hayo yamesemwa na Rais Samia akijibu swali kuhusu namna ya kuvutia vijana kwenye kilimo, upatikanaji wa ardhi, teknolojia na fedha wakati wa ufunguzi wa mkutano unaohusu Kilimo unaofanyika Dakar nchini Senegal.

Pamoja na serikali kujidhatiti, Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB imetangaza kutoa mkopo wa dola za Kimarekani milioni 120 kwa ajili ya sekta ya kilimo ikiwemo umwagiliaji na kujenga kituo cha usafirishaji na usambazaji mbolea

Mpango huo unaolenga vijana na wanawake ujulikanao kwa jina la BBT, 'Ujenzi wa Kesho Bora' umeanzisha mfuko wa dhamana kwa vijana na huduma za mikopo nafuu chini ya Mfuko wa Pembejeo.

Rais Samia amesema Tanzania imeamua kuanzisha mpango huo kutokana na idadi kubwa ya vijana kukosa sifa zinazohitajika na taasisi za fedha wanapoomba mikopo.

Tangu kuanzishwa kwa mpango huo wa BBT miezi Sita iliyopita, tayari imeweza kutenga jumla ya eka 600,000 kwa nchi nzima na shughuli ya kusafisha mashamba hayo imeanza.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages