Breaking

Tuesday, 24 January 2023

POLISI ANAYEDAIWA KUMJERUHI MWANAE KWA VIBOKO AKAMATWA

Picha na SimiyiPress

Na lango la habari

Jeshi la Polisi mkoani Simiyu linamshikilia Askari Polisi PC Abati Benedicto Nkalango ambaye anatuhumiwa kwa kumpiga mtoto wake mwenye umri wa miaka saba na kumsababishia majeraha makubwa.

Akithibitisha tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu ACP Blasius Chatanda amesema kuwa Mnamo 15/01/2023 majira ya saa 11:00 jioni katika Kambi ya Kituo cha Polisi Bariadi Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu askari wa Jeshi la Polisi mwenye namba H- 4178 PC Abati Benedicto Nkalango(27) alimshambulia Mtoto wake aitwaye Benedicto Abati mwenye miaka 7 , mwanafunzi wa darasa la kwanza shule ya msingi Gappa, kwa kumpiga na fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia majeraha makubwa.

Kamanda Chatanda ameeleza kuwa, siku hiyo akiwa nyumbani kwake, alikagua madaftari ya mtoto huyo na kugundua alikuwa amekosa baadhi ya maswali ya hisabati aliyokuwa amepewa Hivyo alimchapa viboko vingi ambavyo hakumbuki idadi na kumsababishia kutokwa damu maeneo ya mgongoni.

"Mtuhumiwa baada ya kufanya ukatili huo kwa mtoto Wake, alichukua dawa na kumpatia matibabu akiwa nyumbani." Ameeleza ACP Chatanda

Hadi sasa mtuhumiwa amekamatwa na anashikiliwa na Jeshi la Polisi wakati taratibu nyingine za kisheria na kinidhamu zinakamilishwa dhidi yake.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages