Polisi katika kaunti ya Kakamega nchini Kenya wamemkamata mwanamke mmoja anayedaiwa kumshambulia mume wake kabla ya kuteketeza nyumba yake kufuatia mzozo wa nyumbani.
Mshukiwa kwa jina Florence Karakacha mwenye umri wa miaka 43 anaripotiwa kumpiga Bramwel Lubanga na hata kurarua sehemu ya mdomo wake kwa tuhuma za kuoa mke wa pili.
Mwanamke huyo ambaye ni mama wa watoto watano kisha aliteketeza nyumba hiyo kabla ya kukimbia hadi kituo cha Polisi cha Ematiha kilicho karibu akidai kuwa ni mumewe aliyekuwa amemshambulia.
Polisi walitokea kumtia mbaroni mume wake lakini baadaye wakapata taarifa kamili kuhusu kilichojiri kutoka kwa majirani na mtoto wa mwanamke huyo - Rayton Lubanga.
Kwa mujibu wa wanafamilia yao, mwanamume huyo aliamua kuoa mke wa pili baada ya kugundua kuwa mke wake wa kwanza alikuwa anachepuka na kaka wa mume wake.
Akithibitisha kisa hicho, OCPD wa Navakholo Richard Omanga amesema kuwa mwanamke huyo anazuiliwa na polisi akisubiri kufikishwa mahakamani.
Via: Tuko News